Hasira za Yanga kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Wagosi wa Kaya Coastal Union zimeishia kwenye basi la Wagosi hao wa Kaya baada ya mashabiki kuamua kulipopoa mawe.
Tukio hilo limetokea nyuma ya uwanja wa Taifa wakati basi lililobeba wachezaji na viongozi wa Coastal Union lilipokuwa likiondoka uwanjani hapo.
Mashabiki waliokuwa wamebeba mawe walianza kulishambulia basi hilo la Coastal na kupasua vioo ambavyo vimemuuza beki wa pembeni Ahmad Juma aliyechanika sehemu ya nyuma ya kichwa.
Hilo ni tukio la pili mfululizo kwa Coastal Union kushambuliwa na mashabiki wa Yanga,kama itakumbukwa msimu uliopita pia mashabiki wa Yanga waliwahi kuishambulia timu hiyo ya kutokea huko Tanga.
Mkurugenzi wa ufundi wa Coastal Union Nassor Binslum akizungumza na Supermariotz amelaani kitendo hicho akisema si kitendo cha uwanamichezo na kinapaswa kulaaniwa na kila mpenda soka.
Kwenye mchezo huo goli la Yanga limefungwa na Didier Kavumbagu wakati lile la Coastal Union likiwekwa wavuni kwa penati na nahodha Jerry Santo.
Mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro aliyevurunda katika mchezo huo alitoa kadi nyekundu kwa Crispin Odula wa Coastal Union na Simon Msuva wa Yanga.
Katika michezo mingine iliyochezwa leo Simba wamepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid bao likifungwa na Harun Chanongo.
Huko Tabora kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Azam FC wamechomoza na ushindi wa mabao 2-0 yakifungwa na Gaudance Mwaikimba na Seif Karihe.
Uwanja wa Sokoine Mbeya City wamewafunga maafande wa Ruvu Shooting 2-1 wakati huko Mkwakwani Mgambo JKT wamewachapa Ashanti United 1-0.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.