Monday, September 30, 2013

Yanga yaibuka na mpango wa kujenga Jangwani City

 
Klabu ya Yanga sasa imeibuka na mpango wa kujenga mji wake eneo la Jangwani utakaoitwa Jangwani City.

Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa klabu hiyo Francis Kifukwe amesema tayari wameomba kuongezwa eneo la ziada ili kujenga mji huo wa kisasa.

Kifukwe amesema mji huo wa Jangwani utakuwa na viwanja mbalimbali vya mazoezi pamoja na uwanja mkubwa utakaobeba watu elfu 40 pamoja na viwanja vingine vidogo vidogo vya mazoezi na vya timu za watoto.

Aidha mji huo utakuwa na maduka mbalimbali ya kufanya shopping,kumbi za starehe na kumbi za mikutano.

Tayari klabu hiyo imepeleka maombi wizara ya ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi ili waweze kuongezewa eneo la kufanya hivyo.

Wenger aichokonoa Chelsea,amjaza upepo Benitez

 
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kocha Rafael Benitez alipewa wakati mgumu amkiwa Chelsea lakini anaamini historia itaonesha kuwa aliwafanyia kazi nzuri.

Benitez, 53, atatua na kikosi chake cha Napoli huko London kesho kukipiga na the Gunners katika mchezo wa Champions League.

Kocha huyo alipewa kibarua cha muda kuinoa Chelsea November mwaka uliopita akiiongoza kuchukua taji la Europa league lakini hakukubalika kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Wenger anasema Benitez hakutendewa vizuri kwakuwa hawakutarajia kuwa iko siku angeifundisha klabu hiyo lakini alifanya vizuri na muda unavyozidi kwenda watakuja kukubali alichokifanya.
 

Benitez,ambaye aliiongoza Chelsea kumaliza nafasi ya tatu katika ligi kuu,aliondoka Stamford Bridge na kukabidhiwa mikoba ya kukinoa kikosi cha Napoli kuanzia mwezi May na hapo kesho ataiongoza klabu hiyo ya Serie A kwenye mchezo wa kundi F dhidi ya Arsenal.

Timu zote zinakutana zikiwa zimeshinda mechi zake za kwanza za kundi hilo linaloongozwa na Arsenal lakini hata katika ligi Napoli wapo nafasi ya pili wakati Arsenal wanaongoza ligi.

UTATA : Torres akabiliwa na kifungo cha mechi 4

Mshambuliaji wa Chelsea Fernando Torres anaweza kukabiliwa na adhabu ya kukosa michezo minne kufuatia kadi nyekundu aliyooneshwa wikiendi iliyopita huko White Hart Lane kwenye mchezo dhidi ya Tottenham.

Tayari kocha wa The Blues Jose Mourinho amemtupia lawama Jan Vertonghen kwa kudanganya mwamuzi Mike Dean kitendo kilichomfanya kumuonesha Torres kadi ya pili ya njano na kufuatiwa na kadi nyekundu.
 

Lakini Torres sasa anakabiliwa na shtaka la kumshika usoni Vertonghen katika picha zinazomuonesha mkono wa Torres ukimshika usoni mchezaji huyo licha ya video kuonesha hakuna tatizo lolote kwa tukio hilo lililomfanya kutolewa nje lakini Torres hana haki ya kukata rufaa kwa mujibu wa kanuni za FA.

Anakabiliwa na makosa ya kinidhamu na atakuwa mchezaji wa kwanza kuhukumiwa na jopo jipya la kamati ya ligi na FA la kupitia video.

Mwamuzi Mike Dean anatakiwa kutolea ufafanuzi kuhusu kadi ya kwanza ya njano ambayo alimpa Torres.
 

Inaonesha kuwa Torres alipewa kadi ya njano kwa tukio la kwanza baada ya filimbi kupigwa na si kwa tukio la pili la mshambiliaji huyo kumshika usoni Vertonghen,tukio ambalo tayari Dean anakiri kuwa hakuliona.

Hiyo inalipeleka suala hilo kwenye kamati hiyo ya kupitia video ambayo inaundwa na waamuzi wa zamani na kama itabainika kosa hilo ni la vurugu,Torres ataongezewa mechi tatu za ziada ambazo jumla itakuwa mechi nne.
 
Kama atakumbwa na adhabu hiyo Torres atakosa mechi dhidi ya Cardiff na Manchester City na pia atakosa mchezo wa Capital One Cup dhidi ya Arsenal,na baadaye mchezo dhidi ya Norwich.

Hii ndio shughuli ya Suarez

Luis Suarez amerejea tena kuitumikia Liverpool katika mchezo ambao waliichapa Sunderland mabao 3-1 huku Suarez akiingia wavuni mara mbili ikiwa ni mara ya kwanza kuichezea klabu hiyo tokea April 21 katika mchezo dhidi ya Chelsea ambapo aliibuka na tukio la kumngáta beki Branislav Ivanovic na kufungiwa mechi 10.

Katika mchezo wa jana amedhihirisha bado yeye ni moto wa kuotea mbali kwa kutupia mabao mawili,na hii ndio shughuli yenyewe huku akishangilia kwa kuonesha picha ya mkewe na mtoto wake Benjamin.
 
 
 
 
 

Mancini mguu sawa Galatasaray

Bosi wa zamani wa Manchester City Roberto Mancini yupo karibu kutua Galatasaray na sasa wapo katika mazungumzo.

Galatasaray,ambayo ilimtimua kocha Fatih Terim wiki iliyopita imethibitisha kwenye mtandano wake wa Twitter kuwa inakutana na kocha huyo MTaliano mwenye miaka 48 huko Istanbul.

Rais wa klabu hiyo Unal Aysal na mtendaji mkuu Lutfi Aribogan wamekutana na Mancini,na klabu hiyo imetuma picha zinazowaonyesha watatu hao wakiwa pamoja.

Mancini alitimuliwa na Manchester City mwezi May ikiwa ni mwaka mmoja tokea ameiongoza klabu hiyo kutwaa taji la ligi kuu ya England huku pia akiiongoza klabu hiyo kutwaa taji la FA.

Timu hiyo ipo kwenye nafasi ya 10 ikiwa na pointi saba ambazo ni pointi 8 nyuma ya vinara wa ligi hiyo Fenerbache.
Itakumbukwa pia katika Champions league walikutana na kisago cha mabao 6-1 kutoka kwa Real Madrid katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi.

Friday, September 27, 2013

Ngassa aonesha jeuri ya pesa,alipa deni la Simba,asema aliyeguswa anaweza kumchangia

Kiungo mshambuliaji wa timu ya Yanga Mrisho Ngassa leo amelipa jumla ya milioni 45,ikiwa ni fedha ya deni la shilingi milioni 30 pamoja na faini ya milioni 15 za klabu ya Simba kwa Shirikisho la Soka nchini TFF ili aweze kuitumikia timu yake kuanzia kesho.

Ngassa ambaye aliambatana na viongozi wa klabu ya Yanga mjumbe wa sekretarieti Partick Naggi, Afisa Habari Baraka Kizuguto na mhasibu Rose Msamila alikabidhi hundi za malipo kwa idara ya fedha ya shirikisho hilo.

Mara baada ya kukabidhi hundi hiyo Ngassa aliongea na waandishi wa habari nje ya ofisi za TFF na kusema ameamua kulilipa deni hilo ili aweze kuitumikia klabu yake, kwakuwa kukosa michezo sita kumemnyima nafasi kuisaidia timu yake.

Ngassa amesema anaomba aeleweke kuwa fedha hizo amezitoa mwenyewe kwenye akaunti yake ya benki na kuwataka wale wote walioguswa na suala hilo wanaweza kumchangia.

Amesema sasa akili yake yote ipo kwenye Ligi Kuu na lengo lake ni kuhakikisha anaisadia timu yake kufanya vizuri na kupata ushindi katika kila mchezo watakaocheza.

Kocha Ernie Brandts kwa sasa ana fursa ya kumtumia mchezaji huyo kwa kuanzia na mchezo wa kesho baada ya kukamilisha adhabu yake aliyopewa ya kukaa nje kwa mechi sita na akulipa kitita cha shilingi milioni 45.

Villas Boas asema hana urafiki na Mourinho,yeye apindua stori


Kocha wa Tottenham Andre Villas-Boas hajali lolote kuhusu kuvunjika kwa mahusiano yake na boss wake wa zamani ambaye sasa anafundisha Chelsea, Jose Mourinho.

Villas-Boas, 35, alifanya kazi chini ya Mourinho kwa miaka saba wakiwa FC Porto, Chelsea na baadaye Inter Milan na anakutana naye kwa mara ya kwanza wakati the Blues itakapokwenda White Hart Lane kesho.
Kocha huyo anasema alikuwa rafiki wa Mourinho wakati huo,urafiki ambao haupo wakati huu.

Hata hivyo Mourinho kwa upande wake hakutaka kuzungumza lolote kuhusu mahusiano yao na AVB akisema hana la kusema lakini akapindua stori akiwaweka Spurs kuwa moja ya timu zinazowania ubingwa.
Amesema mbio za ubingwa sasa zipo kwa timu sita tofauti na miaka ya nyuma mbio hizo ilikuwa kwa timu mbili.

Mourinho anasema wakati akiifundisha Chelsea kwa mara ya kwanza alikuwa anafukuzia ubingwa na Manchester United peke yake lakini sasa mambo yamebadilika kuna timu zipatazo sita wakiwemo Spurs wanaocheza nao kesho.
Timu sita zinazotajwa ni Chelsea,Manchester United,Manchester City,Arsenal,Liverpool na Spurs.

Hizi ndio busara za Balotelli


Mshambuliaji wa AC Milan Mario Balotelli ameomba radhi kwa wachezaji wenzake na mashabiki kwa kadi nyekundu aliyopewa Jumamosi kwenye mchezo wa ligi kuu ya Italia Serie A uliokwisha kwa timu hiyo kuchapwa mabao 2-1 na Napoli.

Mshambuliaji huyo alioneshwa kadi hiyo baada ya kutoa maneno makali kwa mwamuzi Luca Banti na amekumbana na adhabu ya kufungiwa mechi tatu.

Balotelli amesema anaomba radhi kwa wachezaji wenzake kwakuwa kitendo alichokifanya hakiisaidi timu hiyo huku pia akijutia kwa kusema anajihisi ni mkosaji mbele ya mashabiki wanaoijali timu.

Amesema amefanya kosa kwa kutoa maneno makali dhidi ya mwamuzi lakini anasema hataomba radhi kwa kila mmoja isiwe kama ameua mtu.

Baada ya kupewa kadi klabu ya AC Millan iliamua kutokata rufaa kupinga maamuzi ya kufungiwa kwa mshambuliaji huyo na kocha Massimiliano Allegri akasema Balotelli ana miaka 23 sio motto,amefanya kosa linaighalimu timu na mashabiki,inampasa abadili muenendo wake wa tabia.

Tunisia Majanga,Fifa yatishia kushusha rungu


Waziri wa michezo wa Tunisia Tarek Dhiab ametakiwa kuweka mambo sawa kwenye shirikisho la soka la nchi hiyo,FIFA wakionya kuwa serikali kuvuka mipaka yake na kuingia kwenye masuala ya shirikisho hilo ni kitendo kinachotafsiriwa kama serikali kuingilia masuala ya soka.

Dhiab amewashtua wapenda michezo wan chi hiyo ya Africa kaskazini baada ya kuwataka FIFA kulivunja shirikisho la soka la nchi hiyo bila ya kuwepo kwa sababu zozote.

Fifa wamepingana na hilo na kuitaka serikali kukaa mbali na shirikisho la soka au watachukulia ni kitendo cha serikali kuinvilia masuala ya mpira ambayo adhabu yake ni kufungiwa kujihusisha na soka.

Waziri mkuu wa Tunisia Ali Laarayedh ameitisha haraka mkutano wa kuweka sawa mambo ambao utahudhuriwa na wajumbe wa chama cha soka na wawakilishi wa Waziri wa michezo.

Klabu za Tunisi zinashiriki kwenye ligi ya mabingwa na kombe la shirikisho wakati timu ya Taifa itacheza na Cameroon kwenye mchezo wa kuisaka tiketi ya fainali za kombe la dunia 2014.

EPL : Spurs vs Chelsea,Villas Boas vs Mourinho

 
Chelsea na Tottenham Hotspur wanaingia katika majaribu ya kuwania taji la ubingwa wa ligi ya England EPL wakati watakapokutana uso kwa uso kesho huko White Hart Lane.

Timu zote mbili zimefanya usajili wa kuongeza nguvu kwenye vikosi vyao lakini wananza kampeni ya kulisaka taji hilo huku wakikumbuka kukutana mara 149.

Bao lililotumbukizwa wavuni dakika za majeruhi na Paulinho liliipa Spurs ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Cardiff City wikiendi iliyopita na kuifanya ifikishe pointi 12 sawa na Arsenal wakati Chelsea walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fulham na kuwafanya kufikisha pointi 12 ikiwa ni pointi 2 nyuma ya Arsenal na Spurs.

Lakini mchezo huo pia utawakutanisha tena kwa mara nyingine makocha Andre Villas-Boas na Jose Mourinho wanakutana kwa mara ya kwanza katika ligi kuu ya England.

AVB anakutana na timu yake ya zamani ambayo aliwahi kuitumikia kabla ya kuoneshwa mlango wa kutokea na sasa anakutana nayo ikiwa na kocha tofauti lakini anayemfahamu vizuri.

Hata hivyo beki wa kati wa Chelsea David Luiz,ambaye amecheza mechi moja tu ya ligi chini ya Mourinho anasema si sahihi kuigusa mechi hiyo na kusema ni Mourinho dhidi ya Villas Boas hiyo mechi ni Chelsea dhidi ya Tottenham.

Anasema itakuwa mechi kali inayokutanisha mahasimu,ni mchezo ambao kila mmoja atautazama na kila mmoja anataka kucheza mchezo huo.

Thursday, September 26, 2013

Kocha Banyai akana kuikacha Ashanti


Kocha mkuu wa Ashanti United Hassan Banyai amekana kuikacha timu hiyo.

Banyai amesema ameomba ruhusa ya kushughulikia matatizo yake ya kifamilia na ataungana na timu hiyo baada ya mchezo wake na Mtibwa Sugar.

Amesema kumekuwa na maneno mengi yasiyo na ukweli lakini ukweli uko wazi na hata uongozi unafahamu kila kitu kuhusu matatizo yake ya kifamilia na ndio maana aliomba ruhusa na ikakubaliwa.

"Kaka mimi bado ni kocha wa Ashanti,lakini nilipata matatizo ya kifamilia ndio nayashughulikia,kama huamini muulize Mgoyi(Msafiri)Rais wa Ashanti au waulize viongozi wengine watakwambia ukweli kuwa sijaacha wala sijafukuzwa"alisema Banyai.
Kumekuwa na maneno maneno kuwa kocha huyo ameikimbia timu hiyo baada ya kuwa na mwendendo mbovu katika ligi mpaka sasa ikiwa imefungwa mechi tano na kutoka sare mchezo mmoja.

Hata hivyo Banyai amewataka mashabiki kutulia kwakuwa atarejea katika kikosi hicho baada ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.

Ashanti jana ilichukua kipigo kingine katika ligi,ikikubali kuchapwa mabao 2-0 mbele ya Rhino Rangers ya Tabora kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi.

Arsenal,Chelsea uso kwa uso Capital One

Arsenal watakuwa wenyeji wa Chelsea katika mchezo wa raundi ya nne ya michuano ya Capital One.


Arsenal wametinga hatua hiyo baada ya kuwasukuma nje West Bromwich Albion kwa njia ya matuta hapo jana wakati Chelsea walikata tiketi baada ya kuwachapa Swindon Town kwa maboa 2-0 Jumanne.

Manchester United baada ya kuwasukuma nje Liverpool hapo jana sasa watakutana na Norwich City,wakati Manchester City watakuitana na Newcastle.

Mechi hizo zinatarajia kupigwa October 28.

Draw imeamua mechi hizi.
Sunderland v Southampton
Leicester City (II) v Fulham
Birmingham City (II) v Stoke City
Manchester United v Norwich City
Burnley (II) v West Ham United
Arsenal v Chelsea
Tottenham Hotspur v Hull City
Newcastle United v Manchester City

Wednesday, September 25, 2013

Ashanti United,Rhino patachimbika Tabora leo

Leo katika ligi kuu soka Tanzania bara kunapigwa mchezo mmoja tu kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Tabora wakati Ashanti United itakaposhuka dimbani kukipiga na Rhino Rangers.

Timu hizo zote mbili zimepanda daraja msimu huu na zinajua msoto wa ligi daraja la kwanza ili kupanda ligi kuu.

Ashanti angalau walishawahi kuinusa ligi kuu hapo kabla tofauti na Rhino Rangers ambao ni mara yao ya kwanza kuonja utamu wa ligi kuu hivyo hawatakuwa tayari kuukosa kwa kurudi walipotoka huku Ashanti nao wakikumbuka msoto wa kurudi ligi kuu hawatapenda kupoteza nafasi katika wakati ambao wanasota mkiani mwa msimamo wa ligi.

Wauza mitumba hao wa Ilala Ashanti wana pointi moja tu mpaka sasa baada ya kupata sare ya bao 1-1 mbele ya Azam FC lakini imekubali kichapo katika michezo yake yote mingine iliyocheza.

Imechapwa na Yanga 5-1,imefungwa na JKT Ruvu na Mgambo JKT bao 1-0 kila mmoja huku pia ikichapwa na Kagera Sugar katika mchezo uliopita kwa mabao 3-0 kwenye dimba la Kaitaba.

Haye,Tyson sasa kuchapana February


Mabondia David Haye na Tyson Fury sasa watashuka ulingoni February 8 huko jijini Manchester.

Wawili hao walipangiwa kucheza Jumamosi lakini Haye amemumia na kushinwa nyuzi sita.

Haye amewaambiwa mashabiki kuwa bado wataona kile wanachohitaji wakatyi akimchakaza Tyson kwa style ya aina yake.

Tuesday, September 24, 2013

PUMA wamtia kitanzi Usain Bolt


Bingwa wa michuano ya Olympic mkwanariadha Usain Bolt ameongeza mkataba wake na kampuni ya vifaa vya michezo ya Ujerumani PUMA mpaka mwaka 2016 baada ya mashindano yatakayofanyika huko Rio de Janeiro.

Bolt raia wa Jamaica mwenye miaka 27,amekuwa na mkataba na Puma tokea mwaka 2003,na mwanariadha huyo amesema anajivunia kuongeza mkataba na Puma kwa miaka kadhaa.

Mapema alisema kuwa anataka kustaafu mchezo huo baada ya mashindano ya mwaka 2016 lakini sasa amesema anaweza kushindana kwa mwaka mmoja zaidi.

Bolt ameshinda medali sita za dhahabu za Olympic na nane za mashindano ya dunia na rekodi yake yam kukimbia kwa sekunde 9.58 katika mbio za mita 100 inaendelea kusimama mpaka sasa.

Andy Murray afanikiwa oparesheni ya mgongo


Mcheza Tennis namba moja Uingereza Andy Murray ametuma picha yake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akionesha vidole gumba vyake katika ishara ya kwamba yuko sawa baada ya kufanyiwa oparesheni ndogo ya mgongo.

Murray mwenye miaka 26 anatarajia kuanza mazoezi yake ya kabla ya msimu huko Miami mwezi November.

Maumivu hayo aliyofanyiwa oparesheni yalisababisha kutangaza kujiondoa kwenye mashindano ya wazi ya Ufaransa mwezi May lakini akafanikiwa kurejea kwenye michuano ya Wimbledon aliyofanikiwa kushinda na kuwa mchezaji wa kwanza wa kiume kushinda taji hilo tokea mwaka 1936.

Utetezi wake wa US Open iliishia hatua ya robo fainali lakini aliisaidia Great Britain kuifunga Croatia kwenye Davis Cup kabla ya kufanyiwa oparesheni hiyo.

FAINALI ZA AFRICA WANAWAKE : Twiga Stars kuikabili Zambia

Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake Twiga Stars imepangiwa kucheza na Zambia katika mechi za kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake AWC zitakazofanyika mwakani nchini Namibia.

Twiga Stars itaanzia ugenini jijini Lusaka ambapo mechi ya kwanza itachezwa kati ya Februari 13 na 15 mwakani wakati ile ya marudiano itafanyika kati ya Februari 28 na Machi 2 mwakani jijini Dar es Salaam.
Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuitoa Zambia, raundi ya pili ambayo ndiyo ya mwisho itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe. Mechi ya kwanza itakuwa Dar es Salaam kati ya Mei 23 na 25 mwakani wakati ile ya marudiano itakuwa kati ya Juni 6 na 8 mwakani.

Nchi 25 zimeingia katika mashindano huku mabingwa watetezi Equatorial Guinea, makamu bingwa Afrika Kusini na Cameroon iliyoshika nafasi ya tatu katika fainali zilizopita zikiingia moja kwa moja katika raundi ya pili.

Monday, September 23, 2013

Zengwe tupu ngumi za ridhaa,viongozi wadaiwa kujiweka madaraka kinyume na katiba


Shirikisho la ngumi Tanzania BFT limesema halitambui uongozi uliotangazwa kuingia madarakani kukiongoza chama cha ngumi za ridhaa mkoa wa Dar Es Salaam DABA.

Katibu Mkuu wa BFT Makore Mashaga amesema uongozi huo hautambuliki kwakuwa umeingia madarakani kiujanja ujanja bila kuzingatia Sheria na Kanuni za Baraza la Michezo Tanzania BMT , katiba ya Chama cha ngumi cha dunia AIBA, Shirikisho la ngumi Tanzania BFT na katiba ya Chama cha Ngumi mkoa wa Dar es salaam DABA.
Katibu mkuu wa BFT Makore Mashaga
Mashaga amesema Uongozi huo ulijingiza madarakani September 21 2013 katika ukumbi wa DDC Mlimani bila ya kuwa na kibali cha kutoka BFT wala Kibali kutoka Ofisi ya afisa michezo wa mkoa wa Dar es salaam, ambao kiutaratibu ndio walikuwa na mamlaka ya kutoa kibali cha Kufanyika kwa uchaguzi huo na kuusimamia kwa mujibu wa sheria zinazoongoza michezo hapa Tanzania.

Ameongeza kuwa genge la watu wachache walijikusanya na kupeana fomu kinyume na taratibu kwa kujuana na hatimaye kupeana taarifa wakakutana na kujivika madaraka kwa nyadhifa mbalimbali bila kufata taratibu.
Baadhi ya viongozi wanaodaiwa kukiuka katiba
Amesema BFT haikubaliani na jambo hilo kwa kuwa kati ya waratibu wa zoezi hilo waliojivika uongozi wa juu ni wale waliokuwa katika uongozi wa shirikisho la ngumi Tanzania BFT na kupelekea Tanzania kufungiwa uanachama na chama cha ngumi cha dunia AIBA kwa miaka miwili na zaidi kiasi cha kusababisha bondia aliyekuwa tegemeo la Taifa Petro Mtagwa kufungwa jela miaka 15 nchini Mauritius pia kusababisha bondia Emillian Patrick kushindwa kushiriki Mashindano ya Olimpiki 2008 baada ya kuwa amefuzu baada ya kuhusika kula njama za kusafirisha dawa za kulevya.
Mwenyekiti wa uchaguzi wa DABA Zuwena Kipingu akizungumza
Mashanga amefafanua zaidi kuwa wengi wa waliopewa madaraka hawakujzaa fomu za kuomba nafasi kama walivyopewa na hawakuwepo katika uchaguzi huo, wala hawakufanya usaili kama taratibu zilivyo lakini pia wanachama halali waliokuwa wanatakiwa kuwepo katika uchaguzi huo kama viongozi wa chama cha ngumi Temeke hawakupewa taarifa za uchaguzi na wamepeleka  malalamiko ofisi za BFT.

Tamko la BFT ni kwamba uchaguzi huo umekiuka katiba kwa kuhusisha mabondia na viongozi wa ngumi za kulipwa kitu ambacho ni tofauti na katiba zote za ngumi za ridhaa na hivyo BFT itachukua hatua kali za kimaadili na kinidhamu kwa wote waliohusika na zoezi hilo na kusisitiza kwa wanachama wote kuzingatia sheria za uchaguzi wanapofanya uchaguzi wa vyama vyao na kuwataka wengine kutokujiingiza kwa magenge ambayo historia inaonyesha wamekuwa wasubufu wa mambo mbalimbali tokea uongozi wa Narcis Tarimo enzi za TABA kwa masilahi yao binafsi.