Wednesday, September 18, 2013

LIGI KUU : Mbeya City mtoko wa kwanza,Yanga uwanja wa machungu,Simba,Azam nyumbani


Kivumbi cha ligi kuu soka Tanzania bara kinaendelea leo kwenye viwanja 7 ambapo timu 14 zinashuka dimbani kuzisaka pointi tatu muhimu.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga Africa wanashuka dimbani kwenye uwanja ule ule ambao unawakumbusha machungu ya mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City ambao walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 lakini wakalalamika pia kupopolewa mawe na wamekata rufaa kutaka mchezo urudiwe kwenye uwanja huru.

Maafande wa Tanzania Prisons wanaonolewa na kocha Jumanne Challe ambao hawakubaliki sana Mbeya kama walivyo Mbeya City ambao wamepanda daraja msimu huu wameapa watakufa na mabingwa hao watetezi kwenye mchezo huo.

Wekundu wa Msimbazi Simba wao watakuwa kwenye uwanja wake wa Nyumbani uwanja wa Taifa wakiwakaribisha maafande wa Mgambo JKT ambao msimu uliopita waliwangángánia kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Mkwakwani pale Tanga.

Azam FC kwa mara ya kwanza katika msimu huu wanashuka dimbani kuutumia uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex Chamazi wakiwakaribisha vibonde wa ligi mpaka sasa Ashanti United Uncolonized.


Vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu wanaonolewa na Kocha Mbwana Makata watakuwa ugenini Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakicheza dhidi ya ndugu zao wa Ruvu Shooting wanaonolewa na kocha Charles Boniface Mkwasa.


Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar.


Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara ndiye atakayechezesha mechi kati ya Coastal Union na Rhino Rangers itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro ambapo inaikaribisha Mbeya City ya Kocha Juma Mwambusi ambao huo ni mtoko wake wa kwanza tokea kuanza kwa ligi na haijapoteza mchezo wowote mpaka sasa katika mechi zake ilizocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Sokoine.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.