Sunday, September 22, 2013

Yanga yalambishwa Ice cream za Azam Taifa

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania bara Yanga Africa wamekubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Azam FC katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Taifa Dar Es Salaam.

Azam waliandika bao la kwanza katika sekunde ya 29 kupitia kwa John Bocco baada ya kazi nzuri ya Farid Mussa kupiga mpira uliomkuta Brian Umony aliyegonga kichwa kuelekea kwenye lango la Yanga mpira uliookolewa na Kelvin Yondan lakini ukamkuta Bocco aliyepiga kichwa kilichozama wavuni kuhesabu bao la kuongoza kwa Azam lililodumu mpaka mapumziko.

Kipindi cha pili Yanga walikianza kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa mkwaju mkali uliopigwa na Didier Kavumbagu aliyetanguliziwa mpira mzuri na Jerry Tegete.

Yanga wakaongeza bao la pili kupitia kwa mshambuliaji Hamis Kiiza aliyerejea kutoka Lebanon alipokwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa kabla ya Azam FC kusawazisha bao hilo kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Kipre Tchetche baada ya Yondan kuunawa mpira.

Azam wakahitimisha mabao yao kupitia kwa kinda wa miaka 17 Joseph Kimwaga aliyemtungua bao safi Ally Mustapha baada ya kupokea pasi ya Tchetche Kipre katika dakika za nyongeza.

Ushindi huo unamaliza uteja wa Azam kwa Yanga wa kufungwa mechi 4 mfululizo katika siku za hivi karibuni huku Yanga wakishindwa kuifikia rekodi ya Azam kuifunga timu hiyo mara 5 mfululizo.

Azam wamefikisha pointi 9 wakiwa nyuma kwa pointi mbili dhidi ya vinara wa ligi hiyo Wekundu wa Msimbazi Simba wenye pointi 11.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.