Monday, September 23, 2013

Zengwe tupu ngumi za ridhaa,viongozi wadaiwa kujiweka madaraka kinyume na katiba


Shirikisho la ngumi Tanzania BFT limesema halitambui uongozi uliotangazwa kuingia madarakani kukiongoza chama cha ngumi za ridhaa mkoa wa Dar Es Salaam DABA.

Katibu Mkuu wa BFT Makore Mashaga amesema uongozi huo hautambuliki kwakuwa umeingia madarakani kiujanja ujanja bila kuzingatia Sheria na Kanuni za Baraza la Michezo Tanzania BMT , katiba ya Chama cha ngumi cha dunia AIBA, Shirikisho la ngumi Tanzania BFT na katiba ya Chama cha Ngumi mkoa wa Dar es salaam DABA.
Katibu mkuu wa BFT Makore Mashaga
Mashaga amesema Uongozi huo ulijingiza madarakani September 21 2013 katika ukumbi wa DDC Mlimani bila ya kuwa na kibali cha kutoka BFT wala Kibali kutoka Ofisi ya afisa michezo wa mkoa wa Dar es salaam, ambao kiutaratibu ndio walikuwa na mamlaka ya kutoa kibali cha Kufanyika kwa uchaguzi huo na kuusimamia kwa mujibu wa sheria zinazoongoza michezo hapa Tanzania.

Ameongeza kuwa genge la watu wachache walijikusanya na kupeana fomu kinyume na taratibu kwa kujuana na hatimaye kupeana taarifa wakakutana na kujivika madaraka kwa nyadhifa mbalimbali bila kufata taratibu.
Baadhi ya viongozi wanaodaiwa kukiuka katiba
Amesema BFT haikubaliani na jambo hilo kwa kuwa kati ya waratibu wa zoezi hilo waliojivika uongozi wa juu ni wale waliokuwa katika uongozi wa shirikisho la ngumi Tanzania BFT na kupelekea Tanzania kufungiwa uanachama na chama cha ngumi cha dunia AIBA kwa miaka miwili na zaidi kiasi cha kusababisha bondia aliyekuwa tegemeo la Taifa Petro Mtagwa kufungwa jela miaka 15 nchini Mauritius pia kusababisha bondia Emillian Patrick kushindwa kushiriki Mashindano ya Olimpiki 2008 baada ya kuwa amefuzu baada ya kuhusika kula njama za kusafirisha dawa za kulevya.
Mwenyekiti wa uchaguzi wa DABA Zuwena Kipingu akizungumza
Mashanga amefafanua zaidi kuwa wengi wa waliopewa madaraka hawakujzaa fomu za kuomba nafasi kama walivyopewa na hawakuwepo katika uchaguzi huo, wala hawakufanya usaili kama taratibu zilivyo lakini pia wanachama halali waliokuwa wanatakiwa kuwepo katika uchaguzi huo kama viongozi wa chama cha ngumi Temeke hawakupewa taarifa za uchaguzi na wamepeleka  malalamiko ofisi za BFT.

Tamko la BFT ni kwamba uchaguzi huo umekiuka katiba kwa kuhusisha mabondia na viongozi wa ngumi za kulipwa kitu ambacho ni tofauti na katiba zote za ngumi za ridhaa na hivyo BFT itachukua hatua kali za kimaadili na kinidhamu kwa wote waliohusika na zoezi hilo na kusisitiza kwa wanachama wote kuzingatia sheria za uchaguzi wanapofanya uchaguzi wa vyama vyao na kuwataka wengine kutokujiingiza kwa magenge ambayo historia inaonyesha wamekuwa wasubufu wa mambo mbalimbali tokea uongozi wa Narcis Tarimo enzi za TABA kwa masilahi yao binafsi.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.