Tuesday, August 20, 2013

Michezo ya majeshi yazinduliwa Namibia



Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi, Windhoek Namibia.
Hatimaye michezo ya nane kwa majeshi ya Polisi kusini mwa Afrika (SARPCCO GAMES) yamefunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Namibia Dk Hage Geingob katika uwanja wa Taifa wa Namibia na kupambwa na burudani mbalimbali zikiwemo ngoma, nyimbo sarakasi na maonyesho ya helkopta.

Ufunguzi wa mashindano hayo ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi wanachama wa SARPCCO akiwemo IGP Said Mwema.
 

Akizungumza katika ufunguzi huo Dk Geingob alizitaka timu zinazoshiriki mashindano hayo kushindana kwa nidhamu na kudumisha urafiki uliopo ili kuweza kukabiliana na uhalifu kwa kubadilishana mbinu na mikakati kutoka katika mataifa yao kwa lengo la kuwa na ukanda salama wa Kusini mwa Afrika.

Alisema nchi zinashiriki zinahitaji ushindi lakini ni vyema zikatambua kuwa timu moja na bora ndiyo itakayonyakua ushindi kwa kuwa mshindi ni mmoja tu kati ya mataifa yote yaliyoshiriki.

Wakati huohuo Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Said Mwema amewataka wachezaji wa Tanzania kuhakikisha kuwa wanarejea na ushindi ili kupata zawadi nono ambazo amewaaandalia endapo wataibuka na ushindi katika michezo hiyo.

IGP Mwema aliyasema hayo wakati alipowatembelea na kuzungumza na wachezaji wa Tanzania katika hoteli waliyofikia ili kuwapa hamasa na morali wakati wote wa michezo hiyo.

Alisema kitu kikubwa ambacho wachezaji hao wamekifuata nchini Namibia ni ushindi hivyo wahakikishe kuwa wanacheza michezo yote kwa morali na kuibuka na ushindi jambo ambalo litalitea taifa na Jeshi la Polisi sifa.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.