Monday, October 21, 2013

Yanga yamponza Chanongo Simba


Mchezo uliopigwa jana kwenye uwanja wa Taifa katika ligi kuu ya Tanzania bara baina ya mahasimu wa soka la Tanzania Wekundu wa Msimbazi Simba na Yanga Africa umemponza mshambuliaji kinda wa simba Haruna Chanongo na kutemwa kwenye safari ya timu hiyo kwenda Tanga kuikabili Coastal Union hapo Jumatano kwenye uwanja wa Mkwakwani.

Chanongo ameachwa na timu hiyo baada ya kudaiwa kucheza chini ya kiwango kwenye mchezo huo wa hapo jana dhidi ya Yanga uliomalizika kwa sare ya kufungana mabao 3-3 huku Simba wakilazimika kurejea kutoka nyuma na kupata sare hiyo.

Mshambuliaji huyo kinda alitolewa mapema kipindi cha pili na kiungo mwingine Abdulghalim Hamoud na nafasi zao zikachukuliwa na Said Hamis Ndemla na William Lucian.

Hata baada ya mchezo huo kumalizika kocha mkuu Abdallah Kibaden alisema wazi kuwa kiwango kilichooneshwa kipindi cha kwanza na kukubali mabao matatu kilitia mashaka na hata alipoingia kwenye vyumba wakati wa mapumziko aliwaambia wachezaji mabao matatu waliyoachia yanatosha na warudi wakacheze mpira.

Simba wana kibarua hapo Jumatano kukipiga dhidi ya Wagosi wa Kaya Coastal Union ya Tanga kusaka pointi tatu zitakazowarudisha kileleni mwa msimamo wa ligi ambako wamekaa Azam FC wakifuatiwa na Mbeya City ya Mbeya wenye pointi 20 moja zaidi ya Simba wenye pointi 19.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.