Friday, October 4, 2013

Ujenzi wa uwanja wa kombe la dunia wasimama

Kazi ya ujenzi katika Uwanja utakaochezewa mechi za kombe la dunia 2014 nchini Brazil zimesimamishwa baada ya jaji wa mahakama kusema kuna wasiwasi kuhusu usalama.

Uwanja huo wa Arena da Baixada katika jiji la Curitiba ulipangiwa kuchezwa mechi nne za kombe la dunia na ukarabati wa uwanja huo ulikwishacheleweshwa kwa kipindi kadhaa.

Jaji Lorena Colnago amesema maisha ya wafanyikazi yanahatarishwa kutokana na hali ya kuzorota kwa ujenzi huo,akiongeza kusema kuna hatari ya kuzikwa,kukanyagwa na magari na hata kudondoka kutoka kuta za juu za uwanja huo na akaamrisha ukaguzi mpya ufanywe kabla ya kuanza tena shughuli za ujenzi baada ya kugundulika kasoro nyingi katika ujenzi huo.
Taarifa hizo zinakuja wiki moja baada ya uchunguzi kufichua kwamba wafanyakazi walioajiriwa katika ujenzi wa mradi mwingine wa kombe la dunia walikabiliwa na hali ya unyanyasi.

Wachunguzi hao wamesema pia kwamba zaidi ya wafanyakazi 100 walioajiriwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sao Paulo wanaishi katika hali duni karibu na uwanja huo.

Mwezi Agosti, waziri wa michezo Aldo Rebelo alisema ana wasiwasi jinsi ujenzi ulivyochelewa katika viwanja vitano vya michuano ya kombe la dunia mwakani.

Baada ya ziara yake nchini Brazil, katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke,alisema viwanja vyote lazima viwe tayari ifikapo mwezi Desemba na kuonya hatavumilia kuchelewesha ujenzi na hakuna 'mpango mbadala'.

Michuano ya kombe la dunia imepangwa kupigwa katika viwanja 12 nchini kote Brazil.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.