Thursday, October 10, 2013

Kocha aliyevuliwa shati na mashabiki atema kibarua


Kocha wa Levski Sofia aliyevuliwa shati na mashabiki wenye hasira katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari ameitema kazi hiyo siku moja baada ya kupewa kibarua hicho.

Ivaylo Petev, 38,ameachana na kazi hiyo jana katika kile alichokielezea kuchukizwa na kitendo hicho alichofanyiwa.

Mashabiki hao wa Levski waliandamana kwa madai kuwa Petev ana mahusiano na mahasimu wao CSKA Sofia.

Petev mwenyewe anasema ni kitendo cha hovyo ambacho hakivumiliki na hawezi kufanya kazi kwenye mazingira ya aina hiyo,na tayari amefikiria vitu vingi pamoja na kuzungumza na familia.

Anasema si kitu cha kawaida akisema yeye si muuaji,sio mwizi lakini kwa alichofanyiwa na mashabiki hao anasema alichukulia kama amewekwa kwenye kundi hilo.

Wakati ameanza kuzungumza na waandishi wa habari mashabiki wa Levski wakaanza kumbwatukia na kumvua nguo yenye nembo ya klabu hiyo aliyokuwa ameivaa na wakamuonesha mlango wa kutokea.

Petev, anaelezewa kama mmoja wa makocha bora vijana nchini Bulgaria baada ya kuiongoza Ludogorets kuchukua taji la ligi mfululizo.

Mapema mwaka huu Petev ilidaiwa kuwa alisema yeye ni shabiki wa CSKA Sofia lakini mwenyewe anakataa kuwa amewahi kusema hilo kuwa yeye ni mshabiki wa timu hiyo.

Levski tayari wameamua kumtangaza kocha mwingine haraka kuchukua nafasi hiyo,wakimtaja beki wa zamani wa Levski Antoni Zdravkov kama kocha mpya mopaka mwishoni mwa msimu.

Levski, ambao wameshinda taji la ligi nchini Bulgaria mara 26 wapo katika nafasi ya 6 wakiwa na pointi 19,ikiwa ni 9 nyuma ya vinara Ludogorets.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.