Wednesday, October 16, 2013

Bondia wa Tanzania ulingoni kusaka taji la dunia

Bondia Selemani Kidunda wa Tanzania anashuka ulingoni katika uzito wa Welter kutupa karata yake ya kwanza kuusaka ubingwa wa dunia katika masumbwi huko Almaty, Kazakhstan.


Kidunda anacheza na bondia Mandeep Jangra wa India.
 

Mapambano mengine yanayochezwa leo Raytoin Okwiri wa Kenya naye anashuka ulingoni kucheza na Daniel Lewis wa Australia.


Kufikia sasa ni mabondia wawili tu wa Afrika, Efetobor Apochi wa Nigeria uzani wa heavy na Colin Louis wa Mauritius ambao wameshinda mapambano yao na wengine sita kutoka Kenya, Misri, Angola na Nigeria wakashindwa.

Efetobor alimshinda kwa pointi Seyda Keser wa Uturuki naye Louis akamchapa kwa pointi pia Khatuev Salavat wa Norway.

Mabondia sita walioshindwa ni Dan Shisia uzani wa heavy, John Kariuki uzani wa light na Dennis Okoth uzani wa light-welter wote wa Kenya, Vivaldo Rodrigues wa Angola uzani wa fly, Olayinka Yusuff wa Nigeria uzani wa fly na Mohammed Eslam wa Misri uzani wa light-welter aliyeshindwa na Yves Ulysse wa Canada.
Shisia alichapwa na Jim Andreasen wa Denmark kwa pointi, Kariuki akashindwa na Dorjnyambuu Otgondalai wa Mongolia.

Bondia huyo wa Kenya alipata jeraha juu ya jicho lake la kulia hivyo refarii akaamua kuwa hawezi kuendelea na pambano.

Mashabiki wa ndondi mjini Almaty waliachwa vinywa wazi wakishangaa bondia wa Uturuki Fatih Keles alivyomshinda Okoth kwa pointi 2-1.

Makocha wa Kenya Albert Matito na George ''Foreman’’ Onyango wanasema mashabiki waliwazomea majaji kwa uamuzi huo wakisema bondia wa Kenya alistahili kushinda kwa sababu alimuelemea mpinzani wake raundi zote.

Vivaldo Rodrigues wa Angola alishindwa kwa pointi na Malik Jackson wa Marekani uzani wa fly, na bondia mwingine wa Nigeria Olayinka Yusuf akashindwa na Charlie Edwards wa England uzani wa fly.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.