Friday, July 26, 2013

Wanachama wanafki wanarudisha nyuma maendeleo ya soka

Na Frederick Mwakalebela

AMA kweli soka lina maajabu na kila mdau au shabiki wa mchezo huu atakubaliana nami katika hili kwani inaeleweka kabisa. Lakini maajabu ya soka la Tanzania ni tofauti na sehemu zote duniani.
Soka la Tanzania lina maajabu ndani na nje ya uwanja ingawa kwa maajabu ya ndani ya uwanja, hatuwezi kuwashinda ndugu zetu wa Nigeria walioweza kufungana hadi mabao 69-0 ndani ya dakika 90!

Nje ya uwanja ndiko kuna maajabu yake hapa Bong, Kwanza mfumo wa uendeshaji wa klabu zetu ni tofauti sana na kwa wenzetu, lakini kubwa ni pale baadhi ya viongozi wanapoamua kuzifanya klabu kama mali binafsi.

Inawekanaje mtu akajimilikisha, japo kwa muda, klabu kubwa kama Simba au Yanga? Inawezekanaje mtu akajiamulia anavyotaka huku wanaojiita ‘wanachama’ wakipiga makofi?
Wanachama vigeugeu wa aina ya wale tuliowashuhudia Jumamosi kule Police Officers Mess Oysterbay, hawatufai na ni hatari kwa ‘maendeleo endelevu’ ya klabu na soka kwa ujumla.



Nakumbuka kwenye ukumbi huo Yanga nao waliwahi kupiga makofi na kusahau kuuliza muhimu yanayohusu maendeleo ya timu na baadaye wakaanza kuulizana kulikoni.


Presha waliyokuwa wakiisukumaWanachama wakati Simba ikiyumba uwanjani na kutetereka katika duru la pili la Ligi Kuu msimu uliopita, liliwafanya waombe kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wa dharura na Bosi wao, Ismail Aden Rage akagoma. Wakakubaliana naye japo kwa shingo upande kwa kuwa yeye ndiye aliyeshika mpini, wangefanyaje?

Wadaku tukawa tumetega masikio kujua ni nini kitafuata wakati baadhi ya wanachama walipokuwa wakipiga kelele kuwa Mkutano Mkuu Maalumu hauepukiki, tena kwa haraka.
Tukatega masikio hadi yakaanza kuuma, ndipo Rage alipokubali kufanyika kwa mkutano huo. Wale wanachama wakaja juu, wakadai kuwa Katiba ‘imesiginwa’ kwani ‘notice’ ya mkutano haikukidhi vifungu tarajiwa,lakini mwisho waklikubali kwenda mkutanoni.


Siku ya mkutano,Mkutano ukaanza. Loh!!!! Jamaa kimya kama wamenyeshewa mvua. Mwanaume Rage akamwaga sera zake,Kimya! Akaendelea bila hata kuzungumzia kwanini timu imeshika nafasi ya tatu msimu uliopita ilhali iliongoza ligi kipindi kirefu cha mzunguko wa kwanza. Kimya!

Kimya! Kimya! Kimya! Sera zikaendelea (naogopa kuziita porojo) ingawa ule mpango wa ujenzi wa uwanja wa Boko na ukazungumzwa kijuujuu tu tena bila jibu la kuekleweka wakati kwenye mkutano mwingine kama huo ilichangwa shilingi milioni 32 lakini hata majani hajafyekwa.

Mimi nikajiuliza, hawajamaa wamerogwa? Nikajijibu mwenyewe kimya kimya kwamba wanasubiri  tiketi za bure za kwenda kushuhudia mechi ya Simba na URA ya Uganda.

Yaani mbinu iliyotumika wiki moja nyuma kwenye mkutano mwingine maalumu wa TFF, wa kukanyaga vifungu vya ajenda ili muda upite wajumbe wapewe tiketi kwenda kuangalia mechi ya Taifa Stars dhidi ya Cranes (ya Uganda pia), ikatumika tena Jumamosi iliyofuata.

Mkutano ukavunja rekodi ya kuwa mkutano mfupi kuliko yote ya wanachama wa klabu za Simba na Yanga,Wakapewa tiketi (na posho kama ilikuwapo), wakaondoka zao na kuiacha Simba ile ile iliyokuwa kabla ya mkutano.

Cha ajabu walipotoka mkutanoni, wakaanza kupiga mayowe kuwa eti Rage kawaburuza, wengiine wamepiga hodi hadi TFF wakitaka ufafanuzi wa kikatiba! Unafiki mtupu! Mlikuwa wapi wakatimkutano ukiendelea? 


Kitu ambacho nakumbuka Yanga waliwahi kufanya,wakati mkutano mkuu unaendelea nje kulikuwa na mabasi makubwa yanaunguruma yanawasubiri kuwapeleka Morogoro bure na posho mkononi kwenda kutazama mechi yam ligi kwa timu yao,unadhani nini walichokuwa wanawaza wanachama wale zaidi ya kwenda kuitazama timu wanayoipenda.


Wanachama kama hawa hawatufai kabisa na ndio wachawi wakubwa wa maendeleo ya soka letu.

Mwandishi wa makala hii ni katibu mkuu wa zamani wa TFF.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.