Friday, July 19, 2013

Rage omba radhi umeisigina katiba

Na Frederick Mwakalebela

HAPANA shaka sasa ule mkutano mkuu maalumu wa wanachama wa klabu ya Simba umewadia, mkutano uliokuwa ukipigiwa kelele na wanachama hao lakini ukapigwa danadana kwa kuwa Mwenyekiti alikuwa na shughulii nyeti za kitaifa.

Wanachama wa Simba walihitaji mkutano mkuu maalumu mapema mwaka huu wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ilipokuwa ikielekea ukingoni huku timu yao ya soka ikiyumba na kushindwa kuutetea ubingwa wake na hata kushika nafasi ya pili.

Ni kipindi hicho ndipo wanachama hao walikuwa wakiamini kuwa timu ilihitaji usimamizi wa karibu zaidi ya uongozi, kiasi kwamba walitishia kuuondoa madarakani uongozi wa sasa, Mkutano mkuu maalumu haukuitishwa, kisa Mwenyekiti ana shughuli nyingine za kitaifa.

Ni sawa kabisa kwani Mwenyekiti wa Simba pia ndiye Mbunge wa Tabora Mjini na sio ajabu akawa na nyadhifa nyingine mbili au tatu zaidi ya hizo hivyo ni wazi kuwa huwa ana majukumu mengi ya kitaifa na ya binafsi na lazima mkutano mkuu usubiri amalize majukumu hayo kwanza.

Huenda hili la kuuongoza mkutano huo si muhimu sana kwake hata kama klabu hiyo ina maelfu ya wanachama na mamilioni ya mashabiki ndani na nje ya nchi.

Sasa mwenyekiti huyo, Ismael Aden Rage, ameamua kuitisha mkutano mkuu maalumu baada ya kupata muda, tena baada ya kuona kuwa hali sasa ni shwari kwani waliokuwa na jazba wameshasahau machungu ya timu kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, na sasa mkutano unafanyika kesho jijini Dar es Salaam.

Hakika hapo Rage ameisigina Katiba ya klabu hiyo kongwe nchini, Ni Katiba hiyo ambayo aliapa kuilinda na kuisimamia wakati akiingia kwenye uongozi, kwanini amebadilika? Hata mimi sijui.

Katiba ya Simba inamtaka Mwenyekiti kuitisha au kutoa taarifa ya mkutano mkuu siku 30 kabla, lakini ukiangalia safari hii, wito wa mkutano huu ni wa siku 14 tu!

Kana kwamba haitoshi, Mheshimiwa huyo amewapiga pini wanachama wa Simba kwamba wasiwasiliane wala kuzungumza na watu wa vyombo vya habari, Hapo tena ameisigina Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa mtu uhuru wa kuzungumza na kupata taarifa.

Siamini kama Rage, ambaye wakati nikiwa TFF nilifanya naye kazi akiwa Katibu wa Kamati ya Kutunga Katiba za Klabu angeweza kwenda kinyume cha Katiba ambayo ninafahamu kuwa anaielewa vyema kabisa.

Kwa nafasi aliyonayo na heshima yake kwa umma si kwa Wanasimba pekee, Rage alipaswa kuwa ndiye muumini mkubwa na mtu wa kuisimamia katiba na kusimamia utekelezaji wake, Leo ameisigina tena kweupeee!

Rage amebadilika, sasa si mwanademokrasia tena na nina ogopa kutaja jina ambalo angestahili kuitwa kwa sasa.

Kama mdau wa michezo, ninatoa ushauri kwa wanachama wa Simba kwamba pamoja na mapungufu yaliyojitokeza, hawana sababu ya kuugomea mkutano huo wale walio na nafasi waende kuhudhuria bila kukosa hata kama katiba imekiukwa (na ndiyo ukweli).

Waende wakayazungumze yale yaliyo mema kwa maendeleo ya klabu na timu na ninaamini kuwa mambo mengine yatazungumzwa humo humo na kueleweka.

Lakini pia kaka yangu Rage, hebu punguza jazba kidogo, kuwa mpole na ufahamu kuwa huu ni mkutano wa wanachama, si mkutano wa viongozi, Kubali kukosolewa na kuwasikiliza wanachama kwani wao ni sehemu ya klabu, Kumbuka kuwa hata awe Katika nafasi gani, ‘nobody is bigger than Simba Sports Club’.

Jaribu kutumia nafasi ya kesho kwenye mkutano kuwaomba radhi wanachama na kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.


Mwandishi wa makala hii amewahi kuwa katibu mkuu wa shirikisho la soka nchini TFF

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.