Thursday, July 25, 2013

BREAKING NEWS : Sasa si stori tena,Yanga yamalizana rasmi na Kiiza

Sasa si stori tena,mshambuliaji Hamis Kizza Diego raia wa Uganda atavaa jezi za Yanga kwa msimu ujao wa ligi kuu soka Tanzania bara na michuano ya kimataifa.

Kizza leo hii mchana alikuwa na mmoja wa wadau wakubwa wa Yanga aliyewahi kushika moja ya nyadhifa za juu kwenye klabu hiyo ya Yanga na kufanya mazungumzo ambayo kimsingi wamefikia muafaka wa mshambuliaji huyo kutia saini mkataba mpya.

Kizza alikuwa na mdau huyo mwenye nguvu ndani ya klabu hiyo kwenye mmoja wa migahawa maarufu Dar Es Salaam na kufanya mazungumzo hayo ya kina na kufikiwa kwa muafaka.
 
 
Mkataba baina ya Kizza na klabu hiyo ya Yanga utasainiwa kesho na mshambuliaji huyo kuanza kuitumikia tena klabu hiyo,na alikuwa ni mshambuliaji chaguo la kocha Mholanzi Ernest Brandts aliyesisitiza anamuhitaji mshambuliaji huyo na yupo kwenye mipango yake.

Kumalizana na Kizza kunazidi kuipa makali safu ya ushambuliaji ya Yanga ambayo leo imemshusha kikosini mshambuliaji mpya kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro Hussein Javu ambaye tayari ameanza mazoezi asubuhi.

Mkataba wa Kizza ulikwisha na Yanga walikuwa radhi kumuacha aende wakidai anataka dau kubwa lakini baada ya msisitizo wa kocha ndipo usajili wake ukafuatiliwa kiundani na sasa kesho watamaliza kazi ya kusaini mkataba mpya na kumfanya aendelee kuwa mali ya Jangwani kwa mara nyingine.

1 comment:

Note: Only a member of this blog may post a comment.