Friday, July 26, 2013

Azam Media kuonesha live ligi kuu


Azam Media inayomiliki kituo cha Azam TV leo imetangaza udhamini wa kuonyesha michezo ya ligi kuu ya soka Tanzania bara kuanzia msimu ujao ambao umepangwa kuanza kutimua vumbi lake August 24 katika viwanja saba tofauti.

Azam Media wametangaza udhamini huo baada ya kukamilisha mazungumzo ya kina na kamati ya ligi pamoja na vilabu vya ligi kuu yaliyofikia tamati leo katika ofisi za shirikisho la soka nchini TFF.

Uongozi wa Azam media kupitia kwa meneja mkuu wa makampuni ya Salim Said Bakhresa Said Mohamed umekiri kufurahishwa na hatua ya kufanikisha azma ya kuonyesha ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa kushinda zabuni waliyoiwasilisha TFF.

Mohamed amesema dhamira yao ya kutaka kuonyesha ligi kuu ya soka Tanzania bara, ni kupanua wigo wa soka la Bongo ambalo lilikua halipati nafasi kubwa ya kuonekana nje ya mipaka yetu.

Shirikisho la soka nchini TFF kupitia kwa makamu wa kwanza wa Rais Athumani Nyamlani amepongeza juhudi zilizofanywa na uongozi wa Azam Media pamoja na kamati ya ligi.

Nyamlani amesema juhudi ya pande hizo mbili ana hakika zimefanywa kwa ajili ya kuzinufaisha klabu za Tanzania pamoja na watanzania wanaopenda soka.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.