Thursday, July 18, 2013

UCHAGUZI TFF WANUKIA : Tenga ataja kamati za maadili

Rais wa shirikisho la kabumbu nchini TFF Leodger Chillah Tenga ametangaza wajumbe wanaounda kamati ya maadili na kamati ya rufaa ya maadili ikiwa ni sehemu ya kukamilisha agizo lililotolewa na shirikisho la soka duniani FIFA katika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa TFF unaotarajiwa kufanyika mwezi September mwaka huu.

JAJI Steven Ihema na wakili mwandamizi,Jesse Mguto wataongoza kamati muhimu za maadili zilizoundwa baada ya kufanya mabadiliko kwenye katiba ya Shirikisho hilo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Shirikisho hilo pia limemteua Jaji Bernard Luanda kuongoza Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wakati Profesa Mgongo Fimbo ataendelea kuongoza Kamati ya Rufaa za Nidhamu na Kamanda Mstaafu, Alfred Tibaigana akiendelea kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu.

Tenga alisema mabadiliko hayo pia yamegusa kamati nyingine mbili, yaani Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Uchaguzi ambayo sasa itaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Hamidu Mbwezeleni,
Jaji Ihema ataongoza Kamati ya Rufaa za Maadili akisaidiwa na mwanasheria mwingine mwandamizi, Victoria Makani, huku Bi. Mguto, ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza vyombo vya maamuzi ataongoza Kamati ya Maadili akisaidiwa na makamu wake Francis Kabwe, ambaye ni Msajili wa Mahakama Kuu.

Katika uteuzi huo, baadhi ya wajumbe wamehamishwa kutoka kamati moja hadi nyingine. Murtaza Mangungu, ambaye awali alikuwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi, sasa ataingia kwenye Kamati ya Rufaa za Maadili; Kamanda Mohamed Mpinga na Prof Madundo Mtambo wamehamishwa kutoka Kamati ya Rufaa za Uchaguzi kwenda Kamati ya Maadili.

Wajumbe wapya kwenye Kamati hizo ni pamoja na kocha wa zamani wa Taifa Stars na Reli ya Morogoro, Mshindo Msolla na Kamanda Mstaafu Jamal Rwambow wanaingia kwenye Kamati ya Nidhamu.

Mwanasheria Evodi Mmanda anaingia kwenye Kamati ya Maadili, mwanasheria mwandamizi Mustapha Kambona anaingia kwenye Kamati ya Nidhamu,Mohamed Misanga anaingia kwenye Kamati ya Maadili na Kanali Iddi Kipingu, ambaye anasifika kwa kuendesha soka la vijana, anaingia kwenye Kamati ya Rufaa za Nidhamu.

Aidha Mwanasheria Anne Steven Marealle anakuwa mjumbe kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi; Yohane Masale (Rufaa za Uchaguzi), Allen Kasamala (Rufaa za Uchaguzi); Francis Kiwanga ambaye pia aningia kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi na mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau ambaye anaingia kwenye Kamati ya Rufaa za Maadili.

Kamati ya Utendaji pia imefanya mabadiliko kwenye Kamati ya Waamuzi ambako mwenyekiti Said Nassoro na katibu Charles Ndagala wa Chama cha Waamuzi wanaingia kwenye kamati hiyo kushika nafasi ya Joan Minja na Riziki Majala.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.