Wednesday, July 31, 2013

Simba yasajili kifaa kingine

Wekundu wa Msimbazi Simba leo wamekamilisha usajili wa mshambuliaji Betram Mwombeki aliyekuwa anasoma Marekani.

Mshambuliaji huyo alikuwa kwenye majaribio kwa wekundu hao ambao amefaulu na kupewa mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia timu hiyo na ameusaini mbele ya kaimu makamu mwenyekiti Joseph Itangáre Kinesi.

Mwombeki mwenye mwili mkubwa anakumbukwa kwa kutupia bao kwenye mchezo wa kirafiki ambao wekundu hao wa Msimbazi walicheza dhidi ya URA kwenye uwanja wa Taifa Dar Es Salaam.

Simba wanaendelea kuimarisha kikosi chao na safu ya ushambuliaji ikiwa tayari pia imemsajili mshambuliaji kutoka Burundi Hamissi Tambwe.

Valencia yamchokonoa Torres

 
Fernando Torres amepewa ofa ya kuondoka Chelsea na kutua Valencia ya Hispania kwa dau la paundi milioni 20.

Valencia wanataka kutumbukia kwa Torres wakiamini kuwa anaweza kuwa mbadala wa Roberto Soldado anayetakiwa na Spurs.

Bosi wa Valencia Miroslav Duckic alijaribu kutaka kumnasa mshambuliaji wa Arsenal Olivier Giroud, huku pia mshambuliaji wa Real Zaragoza Mreno Helder Postiga akiwa ndiye mshambuliaji anayewezekana kutua kwenye timu hiyo kwasasa.
 
Kukiwa na uwezekano wa kutua kwa mshambuliaji Wayne Rooney kutokea Manchester United inaonekana itampa wakati mgumu Torres ya kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Torres tokea ametua Chelsea kwa dau la paundi milioni 50 mwaka 2011 bado hajaonesha cheche zake akifunga mabao nane kwenye mechi 28 za EPL alizocheza na akitupia jumla ya mabao 23 kwenye mashindano yote akiwa na The Blues.


Ameibuka mfungaji bora kwenye Confederations Cup akiwa na kikosi cha Hispania chini ya Vicente del Bosque.


JEURI YA PESA : Spurs wataka kuifanyia umafia Arsenal,wafikiria kutumbukiza mkono kwa Suarez


Wakati wa usajili kuna wengine huwa wanaachwa na maumivu na kuna wengine huwa wanamaliza kipindi hicho wakiwa wanacheka meno yote nje.

Sasa habari mbaya kwa Arsenal ni kwamba Tottenham wanaweza kuwafanyia umafia mahasimu wao hao wa London Kaskazini na kumchukua Luis Suarez kutoka Liverpool,kama Gareth Bale atakamilisha taratibu za kutua Real Madrid.
 
Tayari Madrid wameweka mezani paundi milioni 85 za kumtaka Bale japo mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy anaweka ngumu anataka paundi milioni 126.

Habari hizo zinaweza kuwa si nzuri kwa mashabiki wa Arsenal ambao wanaamini Suarez ataisaidia timu hiyo japo Liverpool bado wameweka ngumu kumuuza kwa dau la chini ya paundi milioni 50.

Chelsea yahamia kwa Khedira


Real Madid kutumbukia kwa Gareth Bale kumeiamsha Chelsea na sasa inataka kuweka paundi milioni 20 kumnasa kiungo raia wa Ujerumani Sami Khedira.

Madrid wameweka dau la rekodi ya dunia la paundi milioni 85 na hilo linawafanya pia kutaka kutunisha mfuko wao kwa kuuza wachezaji jambo linalomfanya Mourinho kutaka kutumbukia kumnasa Khedira.
 
Mpango huo wa Mourinho unaweza kufanikiwa hasa baada ya kutua kwa kiungo kinda Asier Illarramendi na Isco.


Mourinho anataka kuimarisha kiungo kutokana na kiungo Frank Lampard kukaribia kutundika daruga,Michael Essien anasumbuliwa na maumivu na John Obi Mikel anaweza kuondoka.


Khedira mwenye miaka 26 alijiunga Madrid akitokea Stuttgart mwaka 2010 na amekuwa na mahusiano mazuri na Mourinho.


Madrid watumbukia rasmi na gia kubwa kwa Bale

Real Madrid wametumbukia rasmi na kuweka dau linaloweka rekodi ya dunia katika uhamisho wa wachezaji baada ya kuweka mezani paundi milioni 85 ili kumnasa mshambuliaji wa Tottenham Gareth Bale.

Dau la Real Madrid linaelezwa kuwa lipo mezani kwa karibia wiki sasa ambalo linamchanganya Bale aliyeomba kutaka kuzungumza na wakali hao wa Hispania.
Dau hilo lililowekwa mezani halihusishi mchezaji yeyote wa Real madrid kutolewa kwenda Spurs kama sehemu ya mpango huo.
Tottenham na Bale wamerudi kutoka kwenye Asia Trophy na leo wanarudi mazoezini kujiandaa na msimu mpya wa EPL.

Mchambuzi wa Sky Sports mchezaji wa zamani wa Spurs Jamie Redknapp anasema anafikiri sasa ni wakati wa Bale kuondoka.


Anasema unawezaje kukataa dau kubwa kama hilo huku akiamini klabu hiyo haiwezi kukataa kuuza kwasababu ni kawaida yake akitolea mfano wa Michael Carrick, Luka Modric, na Dimitar Berbatov.
 

Mchezaji ambaye anakamata rekodi ya dunia mpaka sasa ni Cristiano Ronaldo ambaye alitua Madrid mwaka 2009 kwa dau la paundi milioni 80.


Tuesday, July 30, 2013

Lewandowski haendi kokote


Mshambuliaji wa Borussia Dortmund Robert Lewandowski ameahidi kuendelea kucheza Borusia Dortmund kwa moyo wote licha ya kushindikana kuhamia Bayern Munich.

Lewandowski, ambaye mkataba wake na Dortmund unamalizika mwakani amekataa kuongeza mkataba mpya msimu uliopita akisema angejiunga na klabu ya chaguo lake.


Baada ya sakata la mwezi mzima la uhamisho wake na kikaribia kuwa mchezaji wa pili wa Dortmund kunaswa na mahasimu wao Bayern baada ya kufanya hivyo kwa Mario Goetze, Dortmund wakazuia mpango huo.
Mshambuliaji huyo mwenye miaka 24 hajaonesha kuchukizwa na kitendo hicho cha kuzuiwa kuondoka huku akiichezea timu hiyo kwenye mchezo wa German Cup Jumamosi.
 
Lewandowski tayari ana taji la kwanza la msimu baada ya Dortmund kuichapa Bayern kwa mabao 4-2 Jumamosi iliyopita kwenye German Cup.

Mourinho bado anamuota Drogba

Bosi wa CHELSEA Jose Mourinho bado anaendelea kuonesha kuwa anatamani kuungana tena na Didier Drogba huko Stamford Bridge akiwa kama kocha au kama mchezaji.



Drogba, ambaye amebakiza mwaka mmoja kumaliza mkataba wake na Galatasaray,alikuwa kipenzi cha mashabiki huko darajani na anakumbukwa kwa kutumbukiza wavuni penati ya mwisho iliyowapa Chelsea ubingwa wa Ulaya kwenye fainali waliyocheza dhidi ya Bayern Munich.


Drogba mwenye miaka 35 aliitumikia The Blues kwa miaka 8 na Mourinho bado anaendelea kutamani huduma ya mshambuliaji huyo.


Mourinho anasema anafikiri iko siku atarejea Chelsea kwakuwa ni mchezaji muhimu kwenye historia ya klabu hiyo na siku zote ataendelea kubakia kwenye kumbukumbu za mashabiki,uongozi,mmiliki na wachezaji wenzake.
Drogba ametumbukia wavuni mara tano kwenye ligi ya Uturuki.

FC Lupopo mguu sawa kuondoka na Kaseja

Timu ya FC Lupopo ya Congo DRC wapo hatua chache kumnasa golikipa namba moja na nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Starz Juma Kaseja.

Mabosi wa Lupopo wapo hapa nchini tayari kumalizana na Kaseja ili akaanze kuitumikia timu hiyo katika ligi ya Congo.

Lupopo wapo tayari kutoa dau ambalo linatakiwa na golikipa huyo aliyedumu na kuibeba Simba kwa zaidi ya miaka 10 akiwa namba moja na kwenye kikao cha leo na kipa huyo ni kukubaliana baadhi ya mambo ambayo Kaseja ameyataka ili yawekwe kwenye mkataba na kumalizana.
Kaseja mwenyewe anasema baada ya mazungumzo hayo ya leo ndio atajua kama atakwenda kucheza kwenye timu hiyo au ataachana nao japo amekiri kuwa dau ni zuri ambalo limetolewa na timu hiyo na kilichobaki ni kutazama maslahi yake zaidi kama mchezaji.
Kama Kaseja akimalizana na Lupopo kwa makubaliano ya kwenda kucheza huko Congo,atakutana na washambuliaji wa Tanzania wanaocheza Tp Mazembe Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Mkataba wa Simba na Kaseja umemalizika na Simba wamesema kuwa hawana mpango wa kumuongeza mkataba mpya.

KUTOKA Supermariotz blog : Kaseja nabii hakubaliki kwao,bado una kiwango cha juu na kwa umri wako sasa ndio umekomaa na ni wakati wako wa kwenda kupata changamoto mpya kwenye ligi na wachezaji usiowafahamu,kila la kheri.

Monday, July 29, 2013

Bale aitamani Madrid,Spurs wanaendelea kubana

 
Mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy bado anaweka ngumu kuwa Gareth Bale hauzwi licha ya mshambuliaji huyo wa Wales kuonesha anataka kuzungumza na Real Madrid.

Real Madrid wameongeza nia yao ya kumuhitaji lakini Spurs wamechomoa kumuuza Bale hata kwa dau linalowezekana kuweka rekodi ya dunia ya paundi milioni 85.


Real hata hivyo bado hawajawasilisha ofa kimaandishi lakini Bale mwenyewe anataka kutimiza ndoto yake ya kucheza kwa miamba hiyo ya Bernabeu huku mkataba wake ukiwa umebaki miaka mitatu.

Data za Bale msimu kwa msimu EPL

  • 2012-13: Played 33, scored 21, assisted 4
  • 2011-12: Played 36, scored 9, assisted 10
  • 2010-11: Played 30, scored 7, assisted 1
  • 2009-10: Played 23, scored 3, assisted 5
  • 2008-09: Played 16, scored 0, assisted 0
  • 2007-08: Played 8, scored 2, assisted 0

Yanga yaipinga rasmi bodi ya ligi TPL kuipa haki Azam Media kuonesha mechi za ligi kuu

 Mabingwa wa Tanzania Yanga Africa wametangaza rasmi kupinga mechi za ligi kuu soka Tanzania bara kuoneshwa na Azam Media kupitia kituo chake cha televisheni Azam Tv baada ya kupata haki ya kuonesha mechi hizo wakikishinda kituo cha televisheni cha nchini Africa kusini cha Superspot.

Kikao cha kamati ya utendaji cha klabu hiyo kilichoketi jana kimeamua kupinga hatua hiyo ya Azam media kupewa haki hizo za televisheni na bodi ya ligi kuonesha ligi kuu kwa miaka mitatu kutokea msimu ujao utakaoanza kuunguruma August 24.

Mwenyekiti wa Yanga Yusuph Mehboob Manji amesema mkataba huo hauko wazi wenye mgongano wa kimaslahi,kwakuwa kampuni hiyo ndio inayoimiliki Azam FC ambao ni maadui wakubwa wa Yanga uwanjani.
Manji amelalamikia pia bodi hiyo ya ligi ambayo iko kwa mpito kabla ya kufanyika kwa uchaguzi akisema haina mjumbe hata mmoja kutoka klabu ya Yanga.

Bayern Munich kuvunja benki kumnasa Luiz

 

Bayern Munich iko tayari kutoa ofa ya paundi milioni 40 ili kumnasa beki wa Chelsea David Luiz.

Bosi wa Bayern Pep Guardiola alikuwa akihitaji huduma ya beki huyo tokea alipokuwa akiifundisha Barcelona na sasa akiwa kwa mabingwa wa Ulaya yuko tayari kuingia kwenye mbio za kumnasa.

Beki huyo aliyekuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kilichotwaa ubingwa wa Confederation amerejea kujiunga na Chelsea kwenye maandalizi ya kabla ya msimu akiwa chini ya kocha mpya Jose Mourinho na Guardiola anarejea kwenye mbio za kumsajili.


Bayern wamekula kibano cha mabao 4-2 kutoka kwa mahasimu wao Borussia Dortmund kwenye German Super Cup Jumamosi na wanaona bado wanahitaji kuimarisha kikosi.

Inaaminika kuwa Bayern wako tayari kupanda dau mpaka kufikia paundi milioni 45 pamoja na bonasi kitu ambacho ni faida kubwa kwa Chelsea kama wakikubali kwakuwa beki huyo walimnasa kwa dau la paundi milioni 21 kutoka Benfica miaka miwili iliyopita.

Wakati huo huo wachezaji wawili wa zamani wa Chelsea Florent Malouda na Jose Bosingwa leo wanakamilisha kujiunga na Trabzonspor ya Uturuki.

Malouda, 33,aliruhusiwa na Blues kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita wakati Bosingwa, 30 hakuwa na furaha kwenye kikosi cha QPR alichojiunga nacho akitokea Chelsea.

Ana show lov kwa klabu mpya


HAMILTON : Mengi makubwa yanakuja


Dereva wa magari kwenye mashindano ya Formula 1 Langalanga Lewis Hamilton amesema ushindi alioupata kwenye Hungarian Grand Prix ni mmoja wa ushindi muhimu kwenye maisha yake ya mashindano hayo.

Huo ni ubingwa wake wa kwanza tokea amejiunga na timu ya Mercedes,pia ni ushindi wake wa kwanza tokea aliposhinda kwenye United Grand Prix mwezi November.
 

Hamilton anasema ana furaha kubwa kushinda na anaamini mengi makubwa yatafuata baada ya ushindi huo uliofungua njia akiwa na Mercedes.

Kabla ya mashindano hayo Hamilton alikuwa na hofu ya kushindwa kwasababu ya ubora wa matairi lakini baada ya ushindi anasema kama tairi zitaendelea kuwa na ubora huo wanaweza kufanya vizuri kokote.

World championship standings

1 Sebastian Vettel Red Bull 172 points
2 Kimi Raikkonen Lotus 134
3 Fernando Alonso Ferrari 133
4 Lewis Hamilton Mercedes 124
5 Mark Webber Red Bull 105

Sunday, July 28, 2013

BREAKING NEWS : Yanga yapinga Azam Media kuonesha ligi kuu

Kamati ya utendaji ya klabu ya Yanga inakutana muda huu ajenda kubwa ikiwa kupinga Azam Media kupewa haki za kuonesha mechi za ligi kuu soka Tanzania bara msimu ujao.

Kwa mujibu wa mmoja w wajumbe wa kamati hiyo ya utendaji anasema kikubwa wanachotaka kupinga ni kutotangazwa kwa tenda ili washindani wengi zaidi wajitokeze kuwania nafasi hiyo.

Anasema kingine wanachopigania ni kutaka kulipwa fedha zaidi ya vilabu vingine kwakuwa wanaamini wao ni timu kubwa ambayo inaingiza mashabiki wengi zaidi kuliko timu nyingine ambazi hazina mtaji wa mkubwa wa mashabiki.

Hata hivyo kwa mujibu wa sheria ya FIFA haki za kuoneshwa kwa ligi ya nchi husika inamalikiwa na chama cha soka ama shirikisho la nchi hiyo.

Ijumaa Azam Media na kamati ya ligi walitangaza kufikia muafaka wa kusaini mkataba wa miaka mitatu kwa kampuni hiyo ya habari kuonesha mechi za ligi kuu.

Friday, July 26, 2013

Azam Media kuonesha live ligi kuu


Azam Media inayomiliki kituo cha Azam TV leo imetangaza udhamini wa kuonyesha michezo ya ligi kuu ya soka Tanzania bara kuanzia msimu ujao ambao umepangwa kuanza kutimua vumbi lake August 24 katika viwanja saba tofauti.

Azam Media wametangaza udhamini huo baada ya kukamilisha mazungumzo ya kina na kamati ya ligi pamoja na vilabu vya ligi kuu yaliyofikia tamati leo katika ofisi za shirikisho la soka nchini TFF.

Uongozi wa Azam media kupitia kwa meneja mkuu wa makampuni ya Salim Said Bakhresa Said Mohamed umekiri kufurahishwa na hatua ya kufanikisha azma ya kuonyesha ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa kushinda zabuni waliyoiwasilisha TFF.

Mohamed amesema dhamira yao ya kutaka kuonyesha ligi kuu ya soka Tanzania bara, ni kupanua wigo wa soka la Bongo ambalo lilikua halipati nafasi kubwa ya kuonekana nje ya mipaka yetu.

Shirikisho la soka nchini TFF kupitia kwa makamu wa kwanza wa Rais Athumani Nyamlani amepongeza juhudi zilizofanywa na uongozi wa Azam Media pamoja na kamati ya ligi.

Nyamlani amesema juhudi ya pande hizo mbili ana hakika zimefanywa kwa ajili ya kuzinufaisha klabu za Tanzania pamoja na watanzania wanaopenda soka.

Wanachama wanafki wanarudisha nyuma maendeleo ya soka

Na Frederick Mwakalebela

AMA kweli soka lina maajabu na kila mdau au shabiki wa mchezo huu atakubaliana nami katika hili kwani inaeleweka kabisa. Lakini maajabu ya soka la Tanzania ni tofauti na sehemu zote duniani.
Soka la Tanzania lina maajabu ndani na nje ya uwanja ingawa kwa maajabu ya ndani ya uwanja, hatuwezi kuwashinda ndugu zetu wa Nigeria walioweza kufungana hadi mabao 69-0 ndani ya dakika 90!

Nje ya uwanja ndiko kuna maajabu yake hapa Bong, Kwanza mfumo wa uendeshaji wa klabu zetu ni tofauti sana na kwa wenzetu, lakini kubwa ni pale baadhi ya viongozi wanapoamua kuzifanya klabu kama mali binafsi.

Inawekanaje mtu akajimilikisha, japo kwa muda, klabu kubwa kama Simba au Yanga? Inawezekanaje mtu akajiamulia anavyotaka huku wanaojiita ‘wanachama’ wakipiga makofi?
Wanachama vigeugeu wa aina ya wale tuliowashuhudia Jumamosi kule Police Officers Mess Oysterbay, hawatufai na ni hatari kwa ‘maendeleo endelevu’ ya klabu na soka kwa ujumla.



Nakumbuka kwenye ukumbi huo Yanga nao waliwahi kupiga makofi na kusahau kuuliza muhimu yanayohusu maendeleo ya timu na baadaye wakaanza kuulizana kulikoni.


Presha waliyokuwa wakiisukumaWanachama wakati Simba ikiyumba uwanjani na kutetereka katika duru la pili la Ligi Kuu msimu uliopita, liliwafanya waombe kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wa dharura na Bosi wao, Ismail Aden Rage akagoma. Wakakubaliana naye japo kwa shingo upande kwa kuwa yeye ndiye aliyeshika mpini, wangefanyaje?

Wadaku tukawa tumetega masikio kujua ni nini kitafuata wakati baadhi ya wanachama walipokuwa wakipiga kelele kuwa Mkutano Mkuu Maalumu hauepukiki, tena kwa haraka.
Tukatega masikio hadi yakaanza kuuma, ndipo Rage alipokubali kufanyika kwa mkutano huo. Wale wanachama wakaja juu, wakadai kuwa Katiba ‘imesiginwa’ kwani ‘notice’ ya mkutano haikukidhi vifungu tarajiwa,lakini mwisho waklikubali kwenda mkutanoni.


Siku ya mkutano,Mkutano ukaanza. Loh!!!! Jamaa kimya kama wamenyeshewa mvua. Mwanaume Rage akamwaga sera zake,Kimya! Akaendelea bila hata kuzungumzia kwanini timu imeshika nafasi ya tatu msimu uliopita ilhali iliongoza ligi kipindi kirefu cha mzunguko wa kwanza. Kimya!

Kimya! Kimya! Kimya! Sera zikaendelea (naogopa kuziita porojo) ingawa ule mpango wa ujenzi wa uwanja wa Boko na ukazungumzwa kijuujuu tu tena bila jibu la kuekleweka wakati kwenye mkutano mwingine kama huo ilichangwa shilingi milioni 32 lakini hata majani hajafyekwa.

Mimi nikajiuliza, hawajamaa wamerogwa? Nikajijibu mwenyewe kimya kimya kwamba wanasubiri  tiketi za bure za kwenda kushuhudia mechi ya Simba na URA ya Uganda.

Yaani mbinu iliyotumika wiki moja nyuma kwenye mkutano mwingine maalumu wa TFF, wa kukanyaga vifungu vya ajenda ili muda upite wajumbe wapewe tiketi kwenda kuangalia mechi ya Taifa Stars dhidi ya Cranes (ya Uganda pia), ikatumika tena Jumamosi iliyofuata.

Mkutano ukavunja rekodi ya kuwa mkutano mfupi kuliko yote ya wanachama wa klabu za Simba na Yanga,Wakapewa tiketi (na posho kama ilikuwapo), wakaondoka zao na kuiacha Simba ile ile iliyokuwa kabla ya mkutano.

Cha ajabu walipotoka mkutanoni, wakaanza kupiga mayowe kuwa eti Rage kawaburuza, wengiine wamepiga hodi hadi TFF wakitaka ufafanuzi wa kikatiba! Unafiki mtupu! Mlikuwa wapi wakatimkutano ukiendelea? 


Kitu ambacho nakumbuka Yanga waliwahi kufanya,wakati mkutano mkuu unaendelea nje kulikuwa na mabasi makubwa yanaunguruma yanawasubiri kuwapeleka Morogoro bure na posho mkononi kwenda kutazama mechi yam ligi kwa timu yao,unadhani nini walichokuwa wanawaza wanachama wale zaidi ya kwenda kuitazama timu wanayoipenda.


Wanachama kama hawa hawatufai kabisa na ndio wachawi wakubwa wa maendeleo ya soka letu.

Mwandishi wa makala hii ni katibu mkuu wa zamani wa TFF.

Bunduki za Starz kuiua Uganda hizi hapa

Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Starz iliyopo Kampala nchini Uganda kwa mchezo wa kuisaka tiketi ya fainali za mataifa bingwa barani Africa CHAN dhidi ya wenyeji Uganda The Cranes,Kim Paulsen ametaja silaha zake zitakazoanza kesho kuusaka ushindi.

Kim ameamua kumuanzisha kiungo Athuman Idd Chuji ambaye kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa na Starz kulala kwa kufungwa bao 1-0,Chuji alikula benchi na huenda kukosekana kwa kiungo Mwinyi Kazimoto aliyetoroka kambini ikawa imefungua njia ya yeye kuanza.

Stars inatarajiwa kupangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Salum Abubakar, Frank Domayo, John Bocco, Amri Kiemba na Mrisho Ngasa

Moja ya mikakati ya Taifa Stars kwenye mechi hiyo ya keshokushambulia kwa muda mwingi wa mchezo.

Kim amesema maandalizi ya Taifa Stars jijini Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo ambayo Uganda inaongoza kwa bao 1-0 yalikuwa mazuri, lakini mabao ni muhimu hivyo watashambulia bila kusahau kulinda lango lao.

Amesema katika mechi ya kwanza walitengeneza nafasi nyingi lakini hawakuzitumia, hivyo wamekuwa wakifanya mazoezi ya kushambulia, jinsi ya kutengeneza nafasi, na jinsi ya kumalizia.

Amesema angalau kutakuwa na mabadiliko kwa kuingiza sura mbili mpya katika kikosi cha kwanza, na kuongeza kuwa wachezaji wanafahamu umuhimu wa mechi hiyo kwani timu ikienda kwenye Fainali za CHAN itakuwa manufaa kwao binafsi.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefanya mazoezi ya mwisho leo jioni Uwanja wa Mandela ulioko Namboole ambao utatumika kwa ajili ya mechi hiyo kesho.

Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki na itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar wakiongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa mezani (fourth official). Kamishna wa mechi hiyo namba 38 ni Ismail Kamal kutoka Ethiopia.

Kutoka kwa Supermariotz : MUNGU IBARIKI TANZANIA,MUNGU IBARIKI TAIFA  STARZ

Utata wa umri wa Falcao wamalizwa,cheti cha kuzaliwa hadharani

Ubishi wa utata wa umri wa mshambuliaji nyota wa Colombia Radamel Falcao umemalizwa baada ya gazeti moja la Colombia kukiweka hadharani cheti za kuzaliwa cha nyota huyo.

Utata wa umri wake ulikuja baada ya mwalimu mkuu wa zamani wa mshambuliaji huyo kuzungumza kwenye televisheni ya Colombia Noticias Uno akisema Falcao amezaliwa 1984 na sio 1986.

Lakini gazeti la El Tiempo limechapisha cheti za kuzaliwa kutoka manispaa ya Santa Marta kinachoonesha kuwa mshambuliaji huyo kazaliwa February 10, 1986,na hivyo sasa ana umri wa miaka 27 na sio 29.


Nyaraka inayodai Falcao alizaliwa 1984, sio 1986 

Nyaraka kutoka shule ya msingi aliyosoma Falcao
Hii ndio inayothibitisha umri sahihi wa Falcao ikionesha kazaliwa 1986
 Hapa jembe likitambulishwa Monaco
 Jembe kazini na jezi za Monaco
Falcao alitua Monaco ya Ufaransa akitokea Atletico Madrid ya Hispania kwa dau la paundi milioni 53 na kumfanya kuwa mchezaji ghali zaidi kusajiliwa kwenye ligi ya Ufaransa kabla ya Ednson Cavani kuweka rekodi mpya baada ya kusajiliwa na PSG kwa dau la paundi milioni 55.

Thursday, July 25, 2013

BREAKING NEWS : Sasa si stori tena,Yanga yamalizana rasmi na Kiiza

Sasa si stori tena,mshambuliaji Hamis Kizza Diego raia wa Uganda atavaa jezi za Yanga kwa msimu ujao wa ligi kuu soka Tanzania bara na michuano ya kimataifa.

Kizza leo hii mchana alikuwa na mmoja wa wadau wakubwa wa Yanga aliyewahi kushika moja ya nyadhifa za juu kwenye klabu hiyo ya Yanga na kufanya mazungumzo ambayo kimsingi wamefikia muafaka wa mshambuliaji huyo kutia saini mkataba mpya.

Kizza alikuwa na mdau huyo mwenye nguvu ndani ya klabu hiyo kwenye mmoja wa migahawa maarufu Dar Es Salaam na kufanya mazungumzo hayo ya kina na kufikiwa kwa muafaka.
 
 
Mkataba baina ya Kizza na klabu hiyo ya Yanga utasainiwa kesho na mshambuliaji huyo kuanza kuitumikia tena klabu hiyo,na alikuwa ni mshambuliaji chaguo la kocha Mholanzi Ernest Brandts aliyesisitiza anamuhitaji mshambuliaji huyo na yupo kwenye mipango yake.

Kumalizana na Kizza kunazidi kuipa makali safu ya ushambuliaji ya Yanga ambayo leo imemshusha kikosini mshambuliaji mpya kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro Hussein Javu ambaye tayari ameanza mazoezi asubuhi.

Mkataba wa Kizza ulikwisha na Yanga walikuwa radhi kumuacha aende wakidai anataka dau kubwa lakini baada ya msisitizo wa kocha ndipo usajili wake ukafuatiliwa kiundani na sasa kesho watamaliza kazi ya kusaini mkataba mpya na kumfanya aendelee kuwa mali ya Jangwani kwa mara nyingine.