Friday, November 1, 2013

EXCLUSIVE : Masatu akumbuka ya Stella fainali CAF adai hawakuhongwa ...ataja imani za kishirikina zilihusika

Beki kingángánizi,kisiki wa zamani wa Simba na timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars George Magere Masatu amefunguka na kuapa kwa Mungu kuwa mchezo wa fainali ya kombe la CAF mwaka 1993 dhidi ya Stella Abdjan haikuuzwa na wachezaji lakini akakiri ilikuwa na mambo mengi ya kishirikina na imani.

Masatu ambaye enzi za uchezaji wake alikuwa maarufu kwa kuondoa mipira kwenye chaki ya goli amesema mambo yalianzia kwenye mchezo wa kwanza waliocheza huko Ivory Coast na kutoka sare ndipo mambo mengi ya kishirikina na kiimani yalipoanza kuchukua nafasi yake kiasi cha wachezaji kukosa hata muda wa kupumzika.

Masatu anasema watu walikuwa wanapishana kwenye kambi yao huku wachezaji nao wakichukuliwa na kupelekwa sehemu mbalimbali za wataalamu ili kuwaweka sawa kwa mchezo wa marudiano.

Anasema Ijumaa ya siku mbili kabla ya mechi ndio ilikuwa balaa zaidi na mpaka inafika siku ya mechi wachezaji walikuwa hawajapumzika kwa mizunguko hiyo ya kusaka ushindi nje ya uwanja na hata walipoingia uwanjani wakawa wepesi kwa wapinzani wao na hawatamsahau Bolizozo aliyewanyongá na kukosa zawadi ya magari aina ya KIA waliyoahidiwa kama wangetwaa ubingwa.

Masatu anasema kipigo kile kilizua mengo na kuonekana wamehongwa na mfadhili wao wa wakati ule Azim Dewji ili asitoe tena gari hizo za gharama lakini anasema maneno yale yalisaidia kumfanya Azim atoe hata gari ndogo baada ya kukosa ubingwa.

Anaongeza kuwa kitu kingine ambacho kiliwafanya kupoteza mchezo ule mbali na imani hizo ni pamoja na kujiamini kupita kiasi baada ya kupata sare ugenini.

Hata hivyo Masatu amewataka wa Tanzania na wanamichezo wote kiujumla kuamini kuwa mchezo ule haukuuzwa na kilichotokea ni mchezo pamoja na mambo mengine ambayo tayari ameyabainisha,hivyo waelewe kuwa Azim hausiki na wala wachezaji hawakuhongwa.

Masatu anakumbuka enzi zake alipokuwa akifuta mpira kwenye chaki ya mstari wa goli anasema alikuwa anatumia akili ya ziada ambayo washambuliaji walikuwa hawawazi na ndio kilichomfanya kuaminika kama beki bora wa kati kuwahi kutokea hapa nchini.

Akizungumzia kimo chake Masatu anasema ukitumia akili ufupi sio tatizo na ndio maana yeye enzi zake alikuwa anaruka na kupiga mipira ya vichwa kuliko washambuliaji warefu au hata kuliko mabeki wengine warefu.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.