Ligi kuu soka Tanzania bara inaendelea leo kumalizia mzunguko wa kwanza lakini macho na masikio ya wengi yakiwa Azam Complex Chamazi mchezo utakaowakutanisha wenyeji Azam FC dhidi ya Mbeya City.
Mchezo huo una utamu wa aina yake kutokana na vita iliyopo baina ya timu hizo mbili ambazo zipo kileleni na ndizo zitaamua hatima ya timu itakayokaa kileleni wakati mzunguko wa kwanza unamalizika.
Timu hizo zinakutana huku zikiwa ndizo timu pekee ambazo hazijui karaha ya kufungwa katika msimu huu na zikiwa zina pointi 26 kila mmoja.
Kama zitatoka sare na Yanga ikashinda katika mchezo wake dhidi ya JKT Oljoro utakaopigwa uwanja wa Taifa,Yanga watakaa kileleni na kama mmoja wao atashinda ndiye atakayekaa kileleni bila kusikilizia matokeo ya Yanga ambao wana pointi 25 kabla ya mchezo wake wa leo,ikiwa ni pointi moja nyuma ya Azam FC na Mbeya City.
Mchezo huo pia umekuwa na mvuto wa aina yake kutokana na mwenendo wa Mbeya City ambao hakuna timu iliyopata dawa ya kuwafunga na timu iliyobaki kuthibitisha kama ina dawa hiyo ama imekosekana ni Azam FC.
Mvuto mwingine ni kwa timu iliyopanda daraja msimu huu Mbeya City kuonekana kutoa upinzani mkubwa na ikiwa tayari imeweka rekodi ya kushinda mechi sita mfululizo.
Lakini kinachoongeza utamu wa mechi hiyo ni kutokana na matokeo ya mechi tano zilizopita kwa timu hizo ambapo Azam FC imeshinda mechi zote tano zilizopita na Mbeya City pia wameshinda mechi zao zote tano zilizopita.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.