Wednesday, June 18, 2014

Siagi ndio sababu ya unyanya wa Uruguay kombe la dunia Brazil


Wasimamizi wa uwanja wa ndege Brazil wamezuia takriban kilo 39 za siagi ya karameli kutoka timu ya Taifa ya Uruguay walipowasili kwa michezo ya kombe la dunia.

Siagi hiyo ilikamatwa kutoka kwa timu hiyo ilipowasili katika uwanja wa ndege wa Confins karibu na kambi yao wanakofanyia mazoezi,Sete Lagoas.

Siagi hiyo inayojulikana kama ''dulce de leche'' ina umaarufu sana Uruguay lakini wasimamizi Brazil wamesema kuwa kutengenezwa kwake kwa maziwa kunahitaji uhifadhi wa kiwango cha juu cha usafi ambao timu hiyo ya Uruguay haina uwezo wa kutimiza hilo.

Mashabiki wao tayari wameanza kulaumu ulegevu wa timu hiyo iliyochapwa na Costa Rica mabao 3-1 kutokana na ukosefu wa siagi hiyo katika chakula chao.

Msemaji kutoka kitengo cha kilimo cha Brazil amesema timu hiyo inaweza kurudishiwa siagi yao iwapo watakuwa na stakabadhi inayohitajika kuidhinisha kuingia nchini Brazil kinyume cha hapo watalazimika kusubiri hadi baada ya kukamilika kwa fainali hizo.

Mlinda lango wa zamani wa timu hiyo Juan Castillo amesema timu hiyo ilibeba siagi hiyo walipoelekea Afrika Kusini mwaka 2010 na hawakuwa na tatizo lolote la kuzuiwa.

Dulce de leche inatengenezwa kwa maziwa,hamira na vanila na hutumiwa sana kwa kupakwa kwenye mkate,biskuti na kuchanganywa na matunda.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.