Monday, June 30, 2014

Kocha Algeria akerwa na swali la kuhusu wachezaji wanaofunga mfungo wa Ramadhan


Kocha wa timu ya taifa ya Algeria ambayo inashiriki kombe la dunia nchini Brazil, Vahid Halilhodzic amekataa kuweka wazi idadi ya wachezaji wake ambao wanafunga mfungo wa Ramadhan kabla ya mechi yake na Ujerumani inayopigwa leo.

Mfungo huo ambao ni wa siku 30 ulioanza jana Jumapili umemfanya kocha Halilhodzic, mwenye umri wa miaka 61, kukataa kujibu swali kama wachezaji wake watafunga Ramadhan au la wakati wakicheza fainali hizo za kombe la dunia.

Kocha huyo amesema hilo ni swala binafasi na anapoulizwa yeye ni kukosa nidhamu na heshima kwakuwa katika hilo kila mchezaji atafanya anavyotaka.

Mfungo wa Ramadhan ni sharti kwa kila muisilamu na ni moja ya nguzo za imani ya dini ya kiisilamu, ingawa wagonjwa na wazee wanaruhusiwa kutofunga.

Watu ambao wanasafiri au kwenda vitani pia wanaruhusiwa kutofunga ambalo pia linawea kuangukia kwa wanamichezo.

Kocha huyo amesema kuwa si mara ya kwanza kuwa na wachezaji waisilamu katika timu anayofundisha huku akisema yeye mwenyewe ni Muisilamu lakini hawezi kumlazimisha mtu kufuata anachotaka yeye katika dini na huwaacha huru wachezaji kuamua wanachotaka.

Nyota wa timu hiyo Madjid Bougherra, amesema anafunga kama kawaida ingawa mchezaji wa Ujerumani Mesut Ozil na mchezaji wa Ufaransa Bacary Sagna ambao ni waisilamu wamesema hawatafunga.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.