Thursday, May 1, 2014

KISU KWENYE MFUPA : Baada ya Azam kumsajili Domayo,Rais TFF ataka uchunguzi,ampa kazi mwanasheria

Siku moja baada ya Azam FC kuendelea kuibomoa Yanga kwa kumsajili kiungo mkabaji Frank Domayo,Rais wa TFF Jamal Malinzi ameitisha uchunguzi wa mlolongo wa tukio hilo.

Taarifa ya TFF iliyosainiwa na afisa habari wake Boniface Wambura imesema kutokana na tukio lililotokea jana Aprili 30 mwaka huu kwenye kambi ya timu ya Taifa Taifa Stars iliyopo Tukuyu mkoani Mbeya likihusisha usajili wa baadhi ya timu, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF, Jamal Malinzi amemteua Wakili Wilson Ogunde kuchunguza mlolongo mzima wa tukio hilo.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa baada ya kukamilisha uchunguzi wake, Wakili Ogunde ataishauri TFF kuhusu hatua za kisheria na kikanuni za kuchukua.

TFF imetoa wito kwa wachezaji, klabu na wadau wa mpira wa miguu kufuata kanuni na taratibu katika utendaji wao.

Timu ya Mbeya City ndio ilikuwa ya kwanza kufanya usajili kwenye kambi hiyo baada ya kusajili wachezaji wapatao wanne waliopo kwenye mpango wa maboresho ya timu ya Taifa kabla ya Azam nao kutumbukia kwenye kambi hiyo na kuinasa saini ya Domayo aliyemaliza mkataba wake na Yanga uliokuwa wa miaka miwili.

Domayo anakuwa mchezaji wa wa pili ndani ya siku mbili kusajiliwa na Azam FC kutoka kwa mabingwa wa zamani wa Tanzania Bara, Yanga Africa baada ya siku moja kabla klabu hiyo kumsaini mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbangu ambaye pia amemaliza mkataba wake na Yanga.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.