Monday, May 19, 2014

Kamati ya uchaguzi Simba yarudisha wagombea wote,pingamizi kuanza rasmi kesho,watatu wapigwa panga kamati ya uchaguzi


Kamati ya uchaguzi ya wekundu wa msimbazi Simba, imetangaza majina ya awali ya wagombea 40 waliotimiza masharti yaliyowekwa katika fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa klabu hiyo utakaofanyika mwishoni mwa mwezi ujao

Akitangaza majina hayo mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Simba Damas Ndumbaro amesema wagombea wote waliochukua na kurejesha fomu wamepitishwa kwenye hatua ya awali na kuanzia kesho wanachama ruksa kuanza kuwawekea pingamizi ikifuatiwa na usaili.

Aidha kamati hiyo imelaani kitendo cha wagombea kusindikizwa na kundi la wanachama na vikundi vya ngoma wakati wa zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu jambo ambalo linaashiria kuanza kwa kampeni za chini kwa chini.

Ndumbaro amesema kamati yake itakapojiridhisha kutokea tena kwa tukio kama hilo, watawajibika kuchukua hatua kali zaidi za kumuengua mgombea kunako kinyang’anyiro hicho.

Pamoja na mambo mengine Ndumbaro akafafanua ni kwanini wamewapitisha wagombea wote waliochukua fomu na kurejesha fomu wakati wapo wanachama waliobainika kukosa sifa na vigezo vya kugombea.

Inaelezwa kuwa baadhi ya wagombea hawana vyeti vya elimu ya sekondari lakini wapo ambao wanatajwa kuwa bado wanatumikia vifungo mbalimbali licha ya kuwepo upotoshwaji kuwa wagombea hao wamesafishwa kwa masamaha wa Rais wa TFF.

Kama itakumbukwa wakati Rais wa TFF Jamal Emily Malinzi anatangazwa kuwa rais mpya wa shirikisho la mpira wa miguu nchini Octoba 28 mwaka jana, alitangaza kuwasamehe waliokuwa wakikabiliwana na vifungo mbalimbali isipokuwa wale wenye kesi za kula rushwa, kutoa rushwa na kupanga matokeo.

Aidha katika msamaha huo akatanabahisha kuwa hauhusiani na msamaha wa vilabu kwasababu vilabu vina taratibu zake.

Wakati huo huo kamati ya utendaji ya wekundu wa msimbazi Simba imefanya mabadiliko ya kamati yake ya uchaguzi kwa kumuongeza mjumbe mmoja mwanasheria Evodius Mmanda na kuwaengua wengine watatu akiwemo Kassim Dewji na Juma Simba Gadafi.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.