Monday, May 5, 2014

Bodi ya ligi yaangusha rungu kwa Ngassa,Kavumbagu na mwamuzi wa Yanga vs Mgambo


Hatimaye bodi ya ligi imemfungia kwa msimu mzima muamuzi Alex Mahagi aliyechezesha mechi ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara kati ya Mgambo JKT dhidi ya Yanga iliyopigwa huko Mkwakwani jijini Tanga.

Mchezo huo ambao ulimalizika kwa Mgambo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, ulishuhudia kikosi hicho kikicheza pungufu hadi mwisho wa mchezo baada ya Mahagi kumtoa nje Mohamed Neto kwa kadi nyekundu baada ya kukataa kukaguliwa kwa kudaiwa ameficha hirizi ama bisibisi.

Afisa mtendaji mkuu wa bodi ya ligi Silas Mwakibinga amesema mbali na kumfungia muamuzi huyo pia wamefuta adhabu ya kadi nyekundu ambayo ilitolewa kimakosa kutokana na ukweli kuwa muamuzi alivurunda kwa maslahi yake binafsi.

Wakati huo huo bodi ya ligi imempiga faini Mrisho Khalfan Ngassa na Didier Kavumbagu shilingi laki tano kila mmoja kufuatia kitendo cha ushirikina walichokionesha wakati wa mchezo wao wa ligi dhidi ya wekundu wa msimbazi Simba uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ngassa na Kavumbagu aliyesajiliwa hivi karibuni na waoka mikate wa Azam fc wametozwa faini hiyo kutokana na kitendo chao cha kutoa taulo la mlinda mlango wa Simba Ivo Mapunda aliloliweka langoni kwake, jambo ambalo linahusishwa na imani za kishirikina.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.