Wednesday, April 2, 2014

EXCLUSIVE : KASEJA agoma Yanga,ni baada ya tuhuma za kuhujumu kwa kufungisha

GOLIKIPA wa Yanga Juma Kaseja ameigomea Yanga kuingia kambini kwa mchezo wake unaokuja dhidi ya JKT Ruvu utakaopigwa Jumapili baada ya kudaiwa kufungisha kwenye mchezo uliopita wa ligi kuu dhidi ya Mgambo Shooting uliopigwa uwanja wa Mkwakwani huko Tanga.

Baada ya mazoezi ya hapo jana jioni yaliyofanyika viwanja vya Tanganyika Packers Kawe Kaseja aliwafuata viongozi wa benchi la ufundi Kocha Van Der Pluijm,msaidizi wake Boniface Mkwasa na kocha wa makipa Juma Pondamali akiweka msimamo wa kutoingia kambini kutokana na tuhuma hizo anazoshushiwa.

Kaseja aliwaambia wazi kuwa hawezi tena kudaka katika mechi zinazofuata kwakuwa haamini tena ndani ya kikosi hicho.

Hata hivyo kocha wa makipa wa Yanga Pondamali akamwambia anatakiwa kukomaa kwakuwa hata yeye enzi zake kuna mechi aliwahi kulaumiwa lakini akaendelea kuvumilia na kuwajibu uwanjani katika mechi zilizofuata kwa kuonesha kiwango chake bora,hivyo na yeye aendelee kukomaa.

Kaseja akaendelea kushikilia msimamo wake wa kutoingia kambini kwakuwa haoni sababu ya kufanya hivyo na akasisitiza sasa acheze kipa mwingine kwenye mechi zilizosalia.

Tayari kulikuwa na mjadala wa goli alilofungwa Kaseja kwenye mechi dhidi ya Azam FC iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1,bao ambalo lilikuwa la kusawazisha kwa Azam lililofungwa na kinda Kelvin Friday ikidaiwa ni goli alilostahili kuokoa.

Kwenye mechi dhidi ya Mgambo Shooting huko Tanga Yanga ikilala kwa kufungwa mabao 2-1 analalamikiwa kwa kusababisha bao la kwanza la Mgambo baada ya kurudishiwa mpira na beki Kelvin Yondan lakini akaupiga vibaya mpira na kumkuta mfungaji aliyeukwamisha wavuni na kuwafanya baadhi ya viongozi wa klabu hiyo kukasirishwa kwa kiasi kikubwa.

Kaseja mwenyewe amekuwa akisisitiza kipa yeyote kufungwa ni kawaida anashangaa kwake anachukuliwa kama malaika akikaa golini hafungwi.

Kipa mwingine wa timu hiyo Ally Mustapha Barthez ambaye alikuwa kipa chaguo la kwanza naye alipoteza namba yake ya kucheza kama chaguo la kwanza baada ya kukubali kufungwa mabao matatu na Simba kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3 huku Yanga wakiwa wametangulia kwa mabao 3-0 mpaka mapumziko akadaiwa kucheza chini ya kiwango na kuruhusu mabao hayo.

Barthez akapoteza namba yake kwa Deogratius Munishi Dida ambaye akaanza kucheza kama kipa chaguo la kwanza mpaka alipoumia na kulazimika kukaa nje ya uwanja ndipo nafasi ikawa ya Kaseja kucheza kama chaguo la kwanza ikiwa ni baada ya kukaa benchi kwa sehemu kubwa ya mzunguko wa pili na akichukuliwa kama kipa chaguo la tatu au la pili wakati mwingine.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.